Shule Yapewa 29,000/- Elimu Bure

 WAKATI Serikali imeanza kutekeleza mkakati wake wa kutoa elimu bure kwa kila mtoto kuanzia chekechekea mpaka kidato cha nne, imebainika baadhi ya shule zimeambulia Sh. 29,000 kwa mwezi Januari.
 
Katika uchunguzi uliofanywa na Nipashe, imebainika kuwa baadhi ya shule zilipewa mgawo wa fedha ambazo hazitoshelezi hata kwa hitaji moja miongoni mwa vipaumele vya mwongozo wa matumizi ya fedha hizo.
 
Katika uchunguzi huo katika shule za Manispaa ya Temeke, Ilala na Kinondoni jijini Dar es Salaam, shule nyingi zimeambulia kati ya Sh. 29,000 mpaka Sh.179,00 kwa ajili ya matumizi ya mwezi mmoja.
 
Fedha hizo ambazo serikali imezitoa kwa shule za msingi na sekondari ni kwa ajili ya kununulia vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ukarabati wa majengo na miundombinu, uandaaji wa mitihani na gharama za michezo.
Nakala za mgawo huo ambazo zilikutwa zimebandikwa maeneo ya shule kwa ajili ya kusomwa na wananchi, zilionyesha shule iliyopewa kiwango kikubwa cha mgawo ni zile zenye zaidi ya wanafunzi 2000 ambazo zimewekewa kiasi kisichozidi Sh. Mil. 1.5 kwenye akaunti zake.
 
Baadhi ya walimu wamelalamika kazi yao itakuwa ngumu kutokana na fedha hizo kuwa sawa na Sh. 533 kwa kila mwanafunzi, na kwamba haziwezi kumhudumia hata mtoto mmoja kwa siku.
 
Wakizungumza kwa masharti ya kutotaja majina yao, baadhi ya walimu walisema mpaka sasa hawajakwenda benki kuzichukua fedha hizo baada ya kushindwa kujua wazifanyie nini.
 
“Serikali ilisema katika kutekeleza mpango wa elimu bure itatoa ruzuku ya Sh. 15,000 kwa kila mwanafunzi, lakini mambo yamekuwa tofauti, pesa tulizopewa ni kidogo sana... kumhudumia hata mtoto mmoja haiwezekani,” alisema mwalimu mmoja.
 
Alisema kabla ya kupewa mgawo huo, walipewa miongozo ya jinsi ya kutumia kutoka kwa maafisa wa elimu wa Manispaa husika.
 
MUONGOZO WA MATUMIZI
Mwongozo huo ambao umetolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), umewaelekeza walimu kuzigawa pesa hizo katika mafungu matano ya matumizi.
 
Kwenye muongozo huo walimu wametakiwa kutumia asilimia 30 ya pesa hizo kununulia vifaa vya kufundishia na kujifunzia, na asilimia nyingine 30 kwa ajili ya ukarabati wa majengo na miundombinu ya shule.
Aidha, muongozo huo unasema asilimia 20 zinatakiwa kuandalia mitihani, pesa nyigine asilimia 10 kwa ajili ya michezo na zilizobaki kwa kazi ya utawala.
 
UKOKOTOAJI WASHINDIKANA
Kwenye mgawo huo, shule nyingi za msingi zimejikuta zikipata mgawo wa chini kabisa, baadhi zilizokutwa na kiwango hicho kwenye mabano ni Shule ya Msingi Mkundi (29,000), Temeke (160,000), Kigamboni (87,000) na Lions Miburani (179,00).
 
Nyingine ni Shule ya Msingi Mwenge (144,000), Mwangaza (210,000), Reginald Mengi (209,000).
 
Shule iliyopata kiasi kikubwa ni Kinyerezi iliyopewa Sh. 1,470,000.
“Tumejaribu kukokotoa pesa tulizopewa tukagundua kila mtoto amepewa shilingi 533 tu,” alisema mwalimu mwingine ambaye shule yake ilipata mgawo huo. “Tulipozigawa kulingana na muongozo tumeshindwa kabisa kutambua nini tuanze.”
 
Kwa mfano mgawo iliyopata Shule ya Msingi Mkundi wa Sh. 29,000, inatakiwa kutumia kama ifuatavyo:
 
Ununuzi wa vifaa (30%) Sh. 8,700, ukarabati wa majengo na miundombinu (30%) Sh. 8,700, uandaaji wa mitihani (20%) 3,800, michezo (10%) Sh. 2,900 na utawala (10%) sawa na Sh. 2,900.
 
“Mambo ni magumu sana maana tumekabidhiwa mzigo mzito (na) tunapokwenda kwa maafisa elimu watusaidie, wanasema lazima tuhakikishe pesa hizo zinatumika na hakuna michango ya aina yoyote,” alisema mwalimu mwingine.
 
CHANZO: NIPASHE
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.