Ajira 1000 za papo hapo jeshini
RAIS John Magufuli jana alitoa ajira 1000 kwa mgambo, wanajeshi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) pamoja na Jeshi la Wananchi (JWTZ), walioshiriki katika Onyesho la Uwezo wa Medani, lililofanyika jana kwenye Chuo cha Kijeshi Monduli, kwa mara ya kwanza tangu Magufuli awe Rais wa Tano Novemba 5, mwaka jana.
“Nimefurahi sana kuona zoezi hili kwa mara ya kwanza na naagiza
wale wote waliofanikisha zoezi hili kuajiriwa na Jeshi,” alisema Rais
Magufuli ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu.
“Nimeambiwa mpo kati ya 800 hadi 1000, lakini pia nitashirikiana
nanyi kuhakikisha maslahi yenu yanaboreshwa sambamba na kufufua Kambi ya
Nyumbu,” alisema.
Kambi ya Nyumbu ina karakana ya ujenzi wa mitambo ikiwemo magari ya
chapa Nyumbu, lakini shughuli hizo zinaonekana kukosa nguvu katika
miaka ya karibuni.
Alisema historia ya nchi yetu inaonyesha ni jinsi gani JWTZ
walivyoimara katika kuhakikisha nchi inakuwa na ulinzi na usalama kwenye
mipaka ya nchi sambamba na kushiriki mazoezi ya kulinda amani katika
nchi mbalimbali.
Alisema hata wanasiasa wanajivunia ulinzi na usalama wa wanajeshi
pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, hivyo atahakikisha
analinda maslahi ya wanajeshi.
Rais Magufuli pia alimwagiza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Hussein Mwinyi na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kuhakikisha
kunakuwa na kiwanda maalum kwa ajili ya kutengeneza sare za jeshi.
Aidha, aliwataka pia kuhakikisha kunakuwa na kiwanda maalum kwa ajili ya kutengeneza viatu vya jeshi.
Alisema atahakikisha anaboresha maslahi ya Jeshi sambamba na kuwa na vifaa vya kisasa.
Alisema atashirikiana na Jeshi katika kuhakikisha wanajenga uchumi
wa nchi, kwani askari hawahitaji asilimia kumi iliyokithiri katika
rushwa, wala hakuna mtu atakayeiba kama wakishirikiana na raia.
Naye Waziri Wa Ulinzi, Mwinyi alimshukuru Rais Magufuli kwa
kukufika eneo hilo na kujionea silaha mpya na za kisasa, katika
kuboresha Jeshi hilo.
“Pia naimani serikali ya awamu ya tano itaendelea kuboresha
vitendea kazi pamoja na maslahi bora ya wanajeshi, hususan katika kuwapa
mbinu mbalimbali za kivita,” alisema Mwinyi ambaye pia alishika wadhifa
huo katika serikali ya awamu ya nne.
Naye Mkuu Wa Majeshi, Jenerali Devis Mwamunyange alisema kuwa Jeshi
hilo linaendelea kuhakikisha amani na utulivu vinakuwapo pamoja na
kwenda kisasa zaidi.
CHANZO:
NIPASHE