MTU NA KAKA YAKE WAHUKUMIWA MIAKA 20 NA KULIPA FAINI YA SH.270 MILIONI KWA UJANGILI
Mahakama ya Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida, imewahukumu mtu na kaka yake, kutumikia kifungu cha miaka 20 kila mmoja na kulipa fidia ya sh. milioni 270, baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya kukutwa na meno ya tembo, silaha na risasi kinyume cha sheria.
Washitakiwa hao ni Nicodem Mchongareli na Festol Mchongareli, ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 13 ya mwaka jana.
Wanadaiwa kukutwa na meno ya tembo mawili yenye thamani ya sh. milioni 27, bunduki tatu zikiwemo za aina ya Riffle, risasi 25 na maganda yake 15.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Joyce Minde, baada ya upande wa Jamhuri uliokuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Salim Msemo na ule wa utetezi kufunga ushahidi.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Joyce alisema wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa jamhuri ulileta mashahidi watano na washitakiwa baada ya kuonekana wana kesi ya kujibu walijitetea wenyewe.