KWA MARA YA KWANZA WANANCHI WAGOMEA MRADI WA BARABARA
Wananchi wa kijiji cha Chekimaji kata ya masama Rundugai wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wamelalamikia halmashauri ya wilaya hiyo kuharibu mazao ya mpunga kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kilometa thelathini inayojengwa kwa kiwango cha Moramu yenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 bila kuwashirikisha.
Wakizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha wakulima wenye mashamba ya mpunga katika kijiji hicho wanasema wanapinga hatua ya halmashauri hiyo kuharibu mazao hayo na kuchukua maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo bila kushirikishwa
Wamesema jumla ya wananchi 40 wameathirika na ujenzi wa mradi huo ambao unatekelezwa na serikali kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni moja ambapo mashamba ya mpunga yenye ukubwa wa ekari 25.2 yameharibika.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha cheki maji Bw.Selemani Juma amesema wananchi hao wameanza kupata mashaka na kutaka kulipwa fidia ya maeneo yao kutokana na uwepo wa baadhi ya watu wachache ambao maeneo yao yalipitiwa na mradi huo wa barabara kubainika wamejengewa vyoo,wengine wamepatiwa mbegu za mpunga kama fidia.
Akijibu malalamiko hayo mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya hai Bw.Said Mderu amesema kabla ya kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo wananchi walishirikishwa na kuridhia ila kuna baadhi ya watu wachache ambao maeneo yao yamepitiwa na mradi huo wanahitaji kulipwa fidia.
Source: ITV