KIIZA AMKUTA TAMBWE, SIMBA IKIICHAPA JKT RUVU
Simba SC leo wamefanikiwa kupata ushindi wa tatu mfululizo katika ligi kuu ya vodacom baada ya kuwachapa JKT Ruvu goli 2-0 katika mchezo uliochezwa katika uwanja wa Taifa hii leo.
Mchezo huo wa ligi kuu ya vodacom ulishuhudia timu zote zikienda mapumziko wakiwa sare ya bila kufungana huku kila upande wakishambuliana kwa zamu.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwa na mashambuli ya kushtukiza kwa kila upande na kila timu ikicheza kwa tahadhari.
Alikuwa Hamisi Kiiza aliyefungua ukurasa wa mabao hii leo baada ya kuifungia Simba SC goli la 10 msimu huu, likiwa ni goli la kwanza katika mchezo huo likifungwa kwa mkwaju wa penati baada ya Danny Lyanga kuangusha katika eneo la hatari katika dakika ya 52.
Goli hilo la Kiiza linamfanya amfikie Amisi Tambwe mwenye magoli 10 katika msimamo wa orodha ya wafungaji bora wao wakiwa kileleni wakifuatwa kwa karibu na Elius Maguli mwenye magoli 9.
Danny Lyanga aliiandikia Simba SC goli la pili katika dakika ya 61 na kupelekea mchezo kumalizika kwa Simba SC kuibuka na ushindi wa goli 2-0 mbele ya vijana hao wa JKT Ruvu wanao nolewa na Abdallah Kibadeni.