Kesi nne kubwa za ufisadi zaiva



TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema imekamilisha mashauri manne, yaliyotokana na udanganyifu na ubadhirifu.
Sasa inatarajia kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watuhumiwa, huku wakiendelea kukamilisha kesi kubwa 36.
Mashauri hayo manne yaliyoiva ni kesi ya ukwepaji kodi ya Kampuni ya Mafuta ya Lake Oil, kesi ya Hati Fungani inayohusu malipo ya Dola za Marekani milioni sita kwa kampuni iliyodai kusaidia Tanzania kupata mkopo nchini Uingereza, kesi ya Shirika Hodhi la Reli (RAHCO) na kesi ya mabehewa ya kokoto ya Kampuni ya Reli (TRL).
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola alifafanua kuwa kesi ya Lake Oil inahusu udanganyifu na ukwepaji kodi uliofanywa na kampuni hiyo kwa kuuza kwenye soko la ndani mafuta ya petroli lita 17,461,111.58.
Kwa mujibu wa Mlowola, kampuni hiyo ilidanganya mafuta hayo yalisafirishwa kwenda nje ya nchi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Zambia na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 8.5.
“Takukuru tumekamilisha uchunguzi wa shauri hili na mtuhumiwa na washirika wake wamepewa miezi miwili kurejesha fedha zote ambazo serikali ilipata hasara na wakishindwa kutekeleza watafikishwa mahakamani,” alifafanua Mlowola, ambaye aliteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa wa Naibu Mkurugenzi Mkuu, kabla ya kukaimu nafasi ya Mkurugezi Mkuu, baada ya kutenguliwa kwa uteuzi wa Dk Edward Hoseah.
Akizungumzia shauri la Hati Fungani, alisema linahusu malipo ya Dola za Marekani milioni sita kwa Kampuni ya Enterprise Growth Market Advisor (EGMA) kwa madai ya kampuni hiyo kusaidia Tanzania kupata mkopo wa Dola za Marekani milioni 600 kutoka Benki ya Standard ya Uingereza.
Alisema Takukuru imebaini kwamba fedha hizo, zilitakatishwa na watumishi wa umma wasio waaminifu, wakishirikiana na baadhi wa kutoka sekta binafsi, wakifahamu wamezipata fedha hizo kwa njia haramu.
“Tupo kwenye hatua nzuri kukamilisha uchunguzi huu na watuhumiwa wote bila kujali hadhi au nafasi ya mtu pamoja na taasisi zilizohusika watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria,” alieleza kuhusu sakata hilo, ambalo limeihusisha Benki ya Stanbic nchini.
Hivi karibuni, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliitoza faini Stanbic Sh bilioni tatu baada ya kubaini benki hiyo, imefanya miamala ya kutia shaka inayohusu malipo kwa kampuni ya Kitanzania ya EGMA ya Dola za Marekani milioni sita, zilizoingizwa kwenye akaunti ya kampuni hiyo na kutolewa ndani ya muda mfupi.
Stanbic iliwezesha Serikali ya Tanzania kuuza Hati Fungani za Dola milioni 600 (Sh trilioni 1.3) kwa Benki ya Standard Chartered ya Uingereza. Mauzo hayo yalifanyika mwaka 2012 kwa Serikali kwa masharti ya kulipwa riba ya asilimia 1.4; lakini Stanbic tawi la Tanzania iliongeza asilimia moja na hivyo kufanya Serikali ya Tanzania kutakiwa kulipa riba ya asilimia 2.4.
Aidha, Mlowola alisema kesi nyingine inamhusu aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Rahco, Benhadard Tito ambaye hivi karibuni Rais John Magufuli alitengua uteuzi wake kwa tuhuma mbalimbali, zilizokuwa zinamkabili na wanachunguza kesi zinazomhusu.
Alisema katika shirika hilo, kuna ukiukwaji wa sheria na taratibu za kuwapata wazabuni kwenye ujenzi wa reli ya kisasa ya kimataifa (standard gauge), unaosimamiwa na Rahco.
Alisema tayari baadhi ya watuhumiwa kwenye kesi hiyo, wamekamatwa na kuhojiwa akiwamo raia wa Kenya, aliyekuwa muhimu katika mchakato huo wa kumpatia mzabuni, Kanji Muhando na wapo kwenye hatua ya mwisho kukamilisha uchunguzi na wote watakaohusika, watafikishwa mahakamani bila kujali hadhi au nyadhifa zao.
Kuhusu kesi ya mabehewa ya kokoto ya TRL, alisema inahusu ukiukwaji wa Sheria ya Manunuzi ya Umma na Kanuni zake kwenye ununuzi wa mabehewa 25 kutoka kampuni ya Hindustan Engineering and Industries.
“Shauri hili limekamilika uchunguzi wake na kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini kuomba kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani waliobainika kujihusisha na matendo ya rushwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na Kanuni za ununuzi wa umma,” alisema.
Alisema Takukuru wao ni vidole vya kutumbua majipu ya Rais na yeye ni dole gumba, hivyo katika mashauri ambayo rais anayatumbua, anaanza kazi mara moja ikiwemo shauri la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
“Sisi hatuhitaji maombi kama mnavyotakiwa kumuombea Rais katika kazi zake, isipokuwa tunahitaji taarifa kutoka kwa wananchi ili tuweze kuokoa fedha za serikali,” alisisitiza.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.