KAFULIA ASHINDA KESI YAKE MAHAKAMA YASEMA YUPO HURU KABISAA KUFANYA HAYA
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imemuachia huru aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani hapo kwa zaidi ya siku 60 kwa mujibu wa kifungo cha 25 cha kanuni ya adhabu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo
Slivester Kainda, katika kesi iliyokuwa ikimkabili Kafulila akidaiwa
kutoa lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hadija Nyembo.
Akitoa uamuzi huo Kainda alisema: “Kesi hii ni ya muda mrefu sana
na upande wa mashtaka umeshindwa kuleta mashahidi na wakati mashahidi
hao wanaishi hapa Kigoma, hivyo kutokana na upande wa mashtaka kushindwa
kuleta mashahidi ninaifuta kesi hii”.
Hakimu Kainda alifuta kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka
ukioongozwa na wakili wa serikali, Shabani Masanja, kudai mahakamani
hapo kuwa haukua na mashahidi na kuomba ipangwe tarehe nyingine ya kesi
hiyo kutajwa.
“Mheshimiwa kwa leo (jana)hatuna mashahidi, tunaomba mahakama yako
tukufu ipange tarehe nyingine ya kutajwa ili tulete mashahidi,” aliomba
wakili huyo.
Awali akisoma hati ya mashitaka, Wakili wa Serikali, Shabani
Masanja, alidai kuwa, Agosti 1, mwaka 2013, majira ya jioni katika
uwanja wa Rest House, kata ya Nguruka, wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma,
mshtakiwa akiwa Mbunge akiwa kwenye mkutano wa hadhara alitoa lugha ya
matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Nyembo.
Alidai mshtakiwa huyo akiwa kwenye mkutano huo wa hadhara, alitamka
kuwa “Mtu kama Hadija Nyembo unamuokota wapi na kumpa ukuu wa wilaya,
unamchukua shangingi la mjini uko unasema aliwahi kuwa mkuu wa wilaya,
mkuu wa wilaya akija hapa maana yake polisi wa wampigie saluti, kuna
polisi wenye akili hapa kuliko huyu mkuu wa wilaya, wanampigia saluti
basi tu manake hana hakili.”
Alidai lugha hiyo ilimdhalilisha mkuu huyo wa wilaya na kwamba kitendo hicho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Masanja alisema upande wa mashtaka ulipanga kupeleka mahakamani
hapo mashahidi sita na kielelezo kimoja cha CD yenye maneno ya kashfa
yaliyotolewa na mshtakiwa.
CHANZO:
NIPASHE