CWT: RAISI MAGUFULI TUNATAKA MISHAHARA YA WALIMU IPANDE KWA ASILIMIA 100
CHAMA
cha Walimu Tanzania (CWT) kimeiomba serikali ya Dk John Magufuli
kupandisha mishahara ya walimu kwa asilimia 100 katika kipindi hiki
ambacho wanahofia baadhi ya walimu nchini kufukuzwa kazi endapo
watatumia vibaya sehemu ya Sh Bilioni 137 zilizotolewa kugharamia utoaji
wa elimu ya bure.
Ombi
hili lilitolewa na Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Iringa, Stanslaus Mhongole
alipokuwa akizungumza na wanahabari katika salamu zake za kuukaribisha
mwaka mpya ambazo pia zilitolewa na viongozi mbalimbali wa chama hicho
mkoani hapa.
“Hatutaki
kuwapoteza walimu wetu popote pale. Ombi langu tuache tabia ya ununuzi
wa vifaa hewa pindi tutakapopokea fedha hizo kwasababu tabia hiyo ipo;
tukiendelea na tabia hiyo katika serikali hii na kwa kupitia utaratibu
huu mpya wa utoaji wa elimu, hakika tutapoteza kazi,” alisema.
Taarifa
iliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa katika ziara yake
ya kikazi mkoani Lindi hivikaribuni inaonesha serikali imetenga kiasi
hicho cha fedha kwa ajili ya kugharamia utoaji wa elimu bure toka
chekechea hadi kidato cha nne katika kipindi cha Januari hadi Juni,
mwaka huu.