Breaking News: Waziri wa maliasili Prof. Maghembe amsimamisha kazi maofisa misitu nchi nzima
Waziri
wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi
Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Mohammed Kilongo na
Maofisa wa Misitu wa Mikoa nchi nzima kupisha uchunguzi wa upotevu wa
mapato ya Serikali.
Akizungumza
leo na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya Wizara hiyo Dar es Salaam,
Prof. Maghembe amesema agizo hilo limekuja kutokana na ubadhilifu
unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana
na rasilimali za misitu katika Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa
katika mfuko Mkuu wa Serikali.
Ameagiza
pia maofisa hao wote wanaokusanya maduhuri ya Serikali katika Wilaya
watumie muda wa siku kumi kuanzia leo kuhakikisha maduhuri yote
yaliyokusanywa yanapelekwa benki ikiwa ni pamoja na kukabidhi vitabu vya
kukusanyia mapato kinyume cha hapo watachukuliwa hatua kali za
kisheria.
“Wale
district forestry officers wote wapeleke vitabu vyao wanavyokusanyia
maduhuri ya Serikali kwenye ofisi za Kanda, Naibu Katibu Mkuu tusaidie
kuwasiliana na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali ifanye ukaguzi wa
vitabu hivyo ndani ya siku kumi tuhakikishe fedha zinazotakiwa zinaingia
kwenye mfuko wa Serikali, Mtu anakusanya fedha ya Serikali toka mwaka
2004 mpaka leo hajapeleka benki ananeemesha hali yake ya nyumbani,
hili hapana”. Alisisitiza Prof. Maghembe.
Kwa
mujibu wa Waziri Maghembe Bw. Mohammed Kilongo ambaye Idara yake ndiyo
inatoa vitabu kwa ajili ya kukusanya maduhuri ya Serikali katika Mikoa
yote na Wilaya zote nchini analazimika kusimamishwa kazi kupisha
uchunguzi ambapo ukikamilika sheria itachukua mkondo wake bila uonevu
wowote.
Katika
hatua nyingine Waziri huyo wa Maliasili na Utalii amewaagiza pia
Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) kutumia muda wa siku saba
kurudi katika jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii maarufu kama
Mpingo House ambalo walihama mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka jana na
kwenda kupanga katika jengo la NSSF Mafao House lililopo Ilala.
“Wakati
tunajenga nyumba hii hapa, tumejenga jengo hili ni kama jengo la
misitu ndio maana linaitwa Mpingo House kwa maana ni jengo la Misitu,
ninyi wenyewe mmejenga jengo kubwa hili mmemaliza mmehama, Naagiza
jumatatu Desemba 11 muwe mmesharudi katika jengo hili, ghorofa ya tatu
nikija kukagua niwakute, haiwezekani mueleze matatizo yote mliyonayo
muhame nyumba ya Serikali mkapange jengo hapo jirani” Alisema Prof.
Maghembe.
Katika
hatua nyingine ya kuboresha uhifadhi wa Misitu nchini Waziri Maghembe
ameiagiza Idara ya Misitu na Nyuki ya Wizara ya Maliasili kuhakikisha
inajiimarisha katika lengo lake kuu la uhifadhi kwa kushirikiana na
wadau wanaohusika kuhakikisha Mamlaka iliyolengwa ya Uhifadhi Misitu
inakamilika.
“Tunataka
tutoke kwenye Wakala wa Huduma za Misitu (Tanzania Forestry Services
Agency) twende kwenye Mamlaka ya Uhifadhi wa Misitu (Tanzania Forestry
Services Authority) ili tuweze kufanya vizuri zaidi kwenye eneo la
uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini, Katibu Mkuu tunaomba pia
usaidie kufanikisha hili” Alisema Prof Maghembe.
Aliongeza
kuwa wakati wa kuundwa Mamlaka hiyo ni vizuri pia Idara ya Misitu na
Nyuki ya Wizara ya Maliasili ikatenganishwa na kila moja kuwa Idara
kamili kutokana na umuhimu wa kila sekta katika kujenga uchumi wa nchi
kwa kutoa fursa ya kuboresha maeneo hayo na kuongeza pato la taifa.
Ameitaka
pia Idara ya Misitu na nyuki kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS)
kuhakikisha kuwa inaongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kuziba
mianya yote ya ubadhilifu pamoja na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato
na kuboresha vyanzo vilivyopo.
Akizungumzia
mchango wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwenye pato la taifa
Mtendaji Mkuu, Bw. Juma Mgoo amesema katika mwaka huu wa fedha TFS
imeweka makisio ya kukusanya Tsh. Bilioni 88 ambapo mpaka hivi sasa
wameshakusanya zaidi ya asilimia 20 na makisio hayo.
Waziri
Maghembe akizungumzia kuhusu uvamizi kwenye hifadhi za taifa na mapori
ya akiba amewataka wananchi wote waliovamia maeneo ya hifadhi za taifa
kwa ajili ya kuchunga mifugo waondoke ndani ya siku saba zijazo, na
wale walivamia mapori ya akiba kwa shughuli za kilimo na ufugaji
waondoke ndani ya miezi mitatu ijayo.
"Serikali
itawaondoa kwa nguvu wasipotekeleza agizo hili la kuondoka katika
maeneo ya hifadhi za taifa na kwenye mapori ya akiba yaliyohifadhiwa”
Alisisitiza Prof. Maghembe.
Akizungumzia
kuhusu biashara ya Mkaa, Prof. Maghembe amewaagiza wataalamu wa Idara
ya Misitu kusimamia biashara ya mkaa kwa kuzingatia taratibu na sheria
ikiwa ni pamoja na kuzuia usafirishaji wa Mkaa nje ya nchi.
Ameongeza
kuwa nishati ya Mkaa ni muhimu lakini Tanzania ina hifadhi kubwa ya
makaa ya mawe ambapo ameitaka Idara ya Misitu kwa kushirikiana na wadau
wengine kuona ni namna gani ya kuweza kutumia mbadala huo kwa kuzalisha
makaa hayo ya mawe kwa matumizi ya kawaida ili kuokoa misitu nchini.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi
amesema kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Waziri yatafanyiwa kazi
kwakuwa lengo lake ni kuona dhamira ya msingi ya Serikali ya awamu ya
tano inafikiwa ya kubana matumizi, kuongeza mapato ya Serikali na
kuhifadhi maliasili za taifa ikiwemo misitu.
(Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii - www.wizarayamaliasilinautalii.blogspot.com)
Waziri
wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akizungumza
katika kikao na Idara ya Misitu na Nyuki pamoja na Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) katika ukumbi wa Ngorongoro Makao Makuu wa Wizara
hiyo Mpingo House Jijini Dar es Salaam leo tarehe 05 Januari, 2015.
Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
Waziri
wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akizungumza
katika kikao na Idara ya Misitu na Nyuki pamoja na Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) katika ukumbi wa Ngorongoro Makao Makuu wa Wizara
hiyo Mpingo House Jijini Dar es Salaam leo tarehe 05 Januari, 2015.
Kamu
Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Bi. Gladnes Mkamba (wa pili kulia)
akiwasilisha taarifa ya Idara yake kwa Waziri wa Maliasili na Utalii
Prof. Jumanne Maghembe wa (pili kushoto) katika kikao hicho.
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Juma Mgoo
(kulia) akiwasilisha taarifa ya ofisi yake kwa Waziri wa Maliasili
na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kulia).
Sehemu ya wajumbe katika kikao hicho.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi (wa pili kulia) akizungumza katika kikao hicho.