Basata yawapa changamoto wasanii

BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata) limeyataka mashirikisho na vyama vyote vya wasanii nchini kufanya uchaguzi wa viongozi kwa mujibu wa katiba zao ili kuhakikisha sekta ya sanaa inakuwa na mfumo bora wa utawala unaotambulika na kuheshimika miongoni mwa wasanii, wadau na serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza, alisema kabla ya kufanya uchaguzi huo mashirikisho hayo yanatakiwa kulipa ada zao ili kuwa hai kwa ajili ya uchaguzi huo.
“Ieleweke kwamba hakuna chama au shirikisho litakaloruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi bila kuwa hai kwa maana ya kulipa ada zote kama zinavyoelekezwa,”alisema.
Mngereza alisema uchaguzi ufanyike mara moja kabla ya Februari mwaka huu viongozi wapya wawe wamekwishapatikana.
Pia, alizungumzia umuhimu wa wasanii kuhakikisha wamesajiliwa, kuwa na vibali vya kufanya kazi za sanaa na kushiriki kikamilifu kujenga mfumo wa utawala katika sekta ya sanaa utakaokuwa unatumika kama mfumo sahihi na rasmi wa mawasiliano baina ya serikali na wasanii.
Alisema kutokana na huko nyuma serikali kupata ugumu wa kuwasiliana na msanii mmoja mmoja, wanahamasisha umuhimu wa kuanzishwa vyama na mashirikisho ya wasanii na kuwalekeza kujiunga katika umoja huo kwa ajili ya kurahisisha uendeshaji wa sekta hiyo.
Alitaja mashirikisho baadhi yaliyoundwa kuwa ni shirikisho la wasanii wa muziki, ufundi, maonesho na filamu.
“Mashirikisho yote haya yanajumuisha tanzu zote za sanaa na yanaundwa na vyama wanachama ambavyo kimsingi vinaundwa na vikundi vya wasanii na mmoja mmoja kulingana na fani husika,” alisema.
Alisema licha ya kuwa wasanii huhamasika kuunda mashirikisho hayo, bado idadi kubwa ya wasanii hasa wenye majina makubwa wameendelea kuwa nje ya mfumo huo wa utawala katika sekta ya sanaa hali ambayo sio tu imeyafanya maslahi yao kukosa sauti ya pamoja bali pia kudhoofisha juhudi.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.