Gesi yaleta mapinduzi makubwa ya umeme

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kuwa, ifikapo mwezi ujao umeme unaotokana na gesi unaozalishwa nchini utafikia megawati 700 sawa na asilimia 70 ya umeme wote kwenye Gridi ya Taifa. Hayo yatakuwa ni mapinduzi makubwa kwani miaka mingi vyanzo vya maji ndivyo vilikuwa vikichangia kwa asilimia 70.
Aidha, shirika hilo limetoa siku saba kwa wateja wanaojua mita zao zimechezewa, wajisalimishe kwa mameneja wa mikoa kwani baada ya hapo, utafanyika msako kabla ya kuchukuliwa hatua ikiwemo kufilisiwa mali kulipa deni. Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema kuanzia Septemba 17, mwaka huu walipoanza kutumia gesi kutoka mkoani Mtwara, uzalishaji kwa kutumia gesi umeongezeka kutoka megawati 260 hadi 540.
Mramba alisema hilo ni ongezeko la megawati 300 jambo lililosaidia kuboresha hali ya umeme. Alisema wanatarajia kuongeza umeme wa megawati 130 kutoka vyanzo vya gesi kati ya mwezi huu na Januari mwakani na kufanya uongezeke kufikia megawati 700.
“Haya ni mapinduzi makubwa kwani miaka mingi vyanzo vya maji ndivyo vimekuwa vikichangia zaidi ya asilimia 70 ya umeme nchini jambo lililosababisha athari mbalimbali ikitokea ukame,” alieleza Mramba.
Aidha, alisema mkandarasi wa Mradi wa Kinyerezi II wa megawati 240, anatarajia kuanza kazi mwezi huu au ujao kwa kuwa malipo ya awali yameshafanyika na ujenzi utafanywa na mkandarasi kutoka Japan.






Mramba alisema kutokana na miradi mingi mikubwa inayoendelea nchini huku ikitarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka ujao, kutasaidia kupunguza tatizo la kukatika umeme kutokana na mfumo wa usambazaji.
“Nawaomba wateja wetu wakati huu kazi zinapoendelea kuimarisha miundombinu kuwa na subira na uvumilivu kwa usumbufu utakaokuwa unatokea,” alisema na kuongeza kuwa shirika litajitahidi kurekebisha kasoro kwenye miundombinu ya sasa kupunguza usumbufu wakati marekebisho makubwa yakiendelea.
Akizungumzia maofisa waandamizi walioachishwa kazi, Mramba alisema maofisa hao saba wamefukuzwa kazi kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo wizi na ubadhirifu, miongoni mwao wamo mameneja, wahandisi na wahasibu kutoka mikoa mbalimbali.
Alisema hatua hiyo ilichukuliwa takribani miezi miwili iliyopita na wataendelea kufanya hivyo dhidi ya wafanyakazi wanaobainika kujihusisha na vitendo ambavyo ni kero kwa wateja kama vile lugha mbaya, wateja kudaiwa rushwa, kucheleweshwa huduma na ubadhirifu.
Alitaja mikoa ya kishirika hilo ambayo maofisa hao walikuwa wakifanya kazi ni Kagera ambako kwa mujibu wa Mramba, wahusika walifikishwa mahakamani wiki iliyopita. Mingine ni Kondoa Kaskazini, Katavi, Shinyanga na Ilala.
Alisema shirika liko kwenye maandalizi ya kutoa namba maalumu za simu kwa wateja, ambazo watapiga bila malipo kwa ajili ya kutoa taarifa ya vitendo vya wizi na ubadhirifu wa wafanyakazi ili hatua zichukuliwe. Kuhusu msako dhidi ya wezi wa umeme na wanaochezea mita, alisema wote watawekwa hadharani, kisha kuchukuliwa hatua ikiwemo kufilisiwa mali kulipia hasara ambayo shirika limeingia.
“Kwa siku hizo hakutakuwa na hatua lakini baadaye hatua kali zitachukuliwa kwa kufuata sheria ikiwemo kunadi mali zao ili kufidia deni kama huna uwezo wa kulipa,” alisisitiza.
Akizungumzia madai ya kununua nguzo nje ya nchi, Mramba alisema wapo wasambazaji kutoka ndani na nje ya nchi ambao hupatikana kulingana na sheria ya manunuzi, vigezo vya ubora wa nguzo na bei vikizingatiwa.
Katika hatua nyingine, Mramba alisema watashiriki kufanya usafi katika vituo vya kuzalisha umeme, kando ya transfoma na maeneo mengine yenye miundombinu yao ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Uhuru, Desemba 9.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.