TFF kuichongea Algeria Fifa


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa linafuatilia kwa kina madai yalitolewa na Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Boniface Mkwasa (pichani) kuhusu hujuma walizofanyiwa wakiwa nchini Algeria.
Taifa Stars ilirudiana na Algeria katika mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Urusi 2018 na kufungwa 7-0 na kuondolewa kwa kufungwa jumla ya mabao 9-2 baada ya kutoka sare ya 2-2 katika mchezo wa awali kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mkwasa, Taifa Stars ilifanyiwa hujuma kibao ikiwemo kugandishwa uwanja wa ndege kwa muda mrefu bila kupokewa, sehemu ya uwanja kumwagiwa maji na kuwafanya wachezaji wake kuteleza pamoja na mengine mengi.
Akizungumza na gazeti hili jana,Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema kuwa ofisi yake imepata habari kuhusu madai hayo na sasa wanazifanyia kazi. Alisema kuwa baada ya kujiridhisha itawasilisha malalamiko yake kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), lakini kwa sasa ni mapema mno hadi watakapopata ushahidi.
Alisema kuwa ikishapata ushahidi wa kutosha itawasilisha kwa wahusika ili kuzuia hujuma kama hizo kujitokeza. “Sisi kama shirikisho tumesikia hujuma hizo na tunazifanyia kazi kwa kuwa kama ni kweli walitendewa vibaya basi ni dhahiri kuwa haki lazima itendeke,”alisema Mwesigwa. Na Mwandishi Wetu
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.