SERIKALI YA WANAFUNZI CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM (DARUSO) TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MIKOPO KWA WANAFUNZI WA MWAKA WA KWANZA 2015/2016
Ndugu wanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo
kikuu cha Dar es Salaam,wanafunzi wa vyuo vyote nchini na watanzania kwa
ujumla, serikali ya wanafunzi chuo kikuu cha Dar es salaam inapenda
kuwajulisha kuwa inayo taarifa juu ya sintofahamu nzito kuhusu suala la
mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu wa mwaka wa kwanza wa masomo
2015/2016 ambapo idadi kubwa ya wanafunzi waliodahiliwa na vyuo
mbalimbali nchini wamekosa mkopo. Mfano katika chuo kikuu cha Dar es
salaam ni wanafunzi 684 tu waliopata mkopo kati ya wanafunzi zaidi ya
6,000 waliodahiliwa na chuo mwaka wa masomo 2015/2016.
Kutokana na hali hiyo, serikali ya
wanafunzi (DARUSO ) kwa umoja wetu kupitia wizara ya mikopo, tuliamua
kuungana na kuchukua hatua za kukutana na mamlaka husika ili kuhoji na
kushinikiza utolewaji wa haraka wa pesa za mikopo kwa kundi kubwa la
wanafunzi wenye sifa waliokosa mkopo katika chuo kikuu cha Dar es salaam
na Tanzania kwa ujumla ambapo kwa mujibu wa bodi ya mikopo (HESLB)
ilionesha kuwa waliomba mkopo walifikia idadi ya wanafunzi zaidi ya
70,000 na walioonekana kuwa na sifa za kupata mkopo walikuwa 58000.
Lakini katika hali ya kushtua, kushangaza na kusikitisha ni wanafuzi
12,000 pekee ndio waliokuwa wamepatiwa mkopo nchi nzima. Hivyo hatua
zifuatazo zilichukuliwa ili kukabiliana na changamoto hii.Mnamo tarehe 04/11/2014 Serikali ya wanafunzi ikiwakilishwa na kamati maalumu ya viongozi tulifika katika makao makuu ya bodi ya mikopo HESLB na kuzungumza nao kinagaubaga kuhusu uhalisia wa jambo hili na wao wakatupa majibu kuwa walipeleka maombi ya wanafinzi 58000 waliokuwa na sifa za kupata mkopo kwenda wizara ya elimu lakini cha kusikitisha ni kuwa ni wanafunzi 12,000 pekee ndio waliweza kupewa mkopo nchi nzima hivyo kuwalazimu HESLB kutoa mkopo kwa wanafunzi wachache katika kila chuo. Kutokana na majibu haya tulilazimika kuonana na katibu mkuu wa wizara ya elimu ili kujua kulikoni hali hii ikatokea.
Mnamo tarehe 06/11/2015 serikali ya wanafunzi kupitia kamati maalum tumeweza kufika wizara ya elimu na kukutana na kaimu mkurugenzi wa masuala ya elimu ya juu Dr. Mbwambo na kuzungumzia suala hili naye akatupa majibu yaliyokuwa pacha na majibu yaliyotolewa na bodi ya mikopo kuwa kulikuwa na upungufu wa fedha zinazofikia kiasi cha billion 132 ili kuwezesha wanafunzi wote nchini wenye sifa za kupata mkopo waweze kunufaika na mkopo huo, hivyo kutokana na maelezo hayo tulilazimika kuonana na katibu mkuu wa wizara ya elimu ili kuweza kujua ni hatua zipi zimechukuliwa ili kuweza kupata kiasi hicho cha fedha kilichopungua. Lakini tunasikitika kuwa hatukuweza kukutana na katibu mkuu licha ya ukweli kwamba tuliweza kuacha ujumbe wetu kwa katibu wake binafsi. Baada ya hatua hii tuliona ipo sababu pia ya kujua ni nini kinachowakwamisha hazina kutoa pesa hizo.
Hivyo siku hiyo hiyo ya tarehe 06/11/2015 tulifika katika ofisi za hazina na kuzungumza na kamishina wa bajeti nae akatuomba tumpe mda wa kufanya kikao na watendaji wa wizara ya elimu pamoja na bodi ya mikopo na akaahidi kutupa majibu kwa njia ya simu siku hiyohiyo ya tarehe 06/11/2015 mara tuu baada ya kikao.
Hivyo, waziri wa mikopo chuo kikuu cha Dar es salaam MH SHITINDI VENANCE ameweza kupokea simu ya mkononi kutoka kamishina wa bajeti nchini tarehe 06/11/2015 muda wa saa 12:25 jioni na alimpa taarifa kuwa katika kikao cha kamishna na bodi ya mikopo pamoja na wizara ya elimu wameafikiana kutoa fedha ndani ya masaa 48 kwa wanafunzi wote nchini wenye sifa na vigezo vya kupata mkopo lakini majina yao hayakuwamo katika majina yaliyokuwa yametajwa hapo awali.
Hivyo wizara ya mikopo katika selikali ya wanafunzi chuo kikuu cha Dar es salaam(DARUSO) Inapenda kuwatangazia wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza katika chuo kikuu cha Dar es salaam na Tanzania kwa ujumla kuwa tutaendelea kusimamia kila hatua mpaka hatua ya mwisho ya mchakato huu pale pesa zenu zitakapo patikana ili muweze kuipata elimu ya chuo kikuu pasi na kikwazo chochote.
IMETOLEWA NA SERIKALI YA WANAFUNZI CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM (DARUSO)
UNITY IS POWER.