Kiiza ajichuja ufungaji bora


WAKATI mshambuliaji Mzimbabwe wa Yanga, Donald Ngoma akitamba ataibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, mshambuliaji wa Simba, Mganda Hamis Kiiza amesema yeye hicho sio kipaumbele chake.
Jana Ngoma alikaririwa na gazeti hili akisema bado hajaona mpinzani wa kumzuia ashindwe kubeba tuzo ya Mfungaji Bora msimu huu baada ya kuizoea Ligi ya Tanzania Bara kwa muda mfupi tangu ajiunge na timu hiyo.
Ngoma alieleza kuwa ametoa kauli hiyo kwa sababu tayari amerudi kwenye kiwango chake alichokizoea, hivyo hafikirii kupata upinzani utakaomfanya ashindwe kutimiza lengo alilojiwekea.
Mzimbabwe huyo alisema anataka kuutumia msimu wake huu wa kwanza kuweka rekodi ya kuwa mfungaji bora kwa kuwa anajua siku zijazo atakuwa na wakati mgumu, zaidi ilivyokuwa wakati anatua kwenye Yanga kwa sababu mabeki wengi watakuwa wanajua madhara yake. Lakini maoni ya Ngoma ni tofauti na Kiiza, ambaye akizungumza na gazeti hili alisema ubingwa ndiyo kipaumbele chake cha kwanza kuliko jambo jingine lolote.
Alisema wakati anasaini mkataba wa kuichezea Simba aliwaahidi mashabiki kwamba anataka kuwapa raha ya ubingwa na hakuwa na mawazo ya ufungaji bora.
Kiiza aliyegeuka kipenzi cha mashabiki wa Simba kutokana na uwezo mkubwa wa kufunga mabao, alisema amekuwa akionesha jitihada hizo kwa ajili ya kutimiza ahadi zake kwa mashabiki na siyo kitu kingine kama watu wanavyofikiria.
“Watu wanafikiri nataka tuzo ya mfungaji bora kitu ambacho siyo kweli, lengo langu kubwa ni kuipa ubingwa wa Tanzania Bara Simba, ndiyo sababu ya kucheza kwa juhudi na kushirikiana na wenzangu ili kutimiza kile nilichoahidi,” alisema Kiiza.
Mshambuliaji huyo aliyewahi kung’ara na Yanga, alisema pamoja na Simba kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 21, bado ana matumaini ya kutimiza lengo hilo kwani tofauti yao na timu inayoongoza ligi ni pointi nne.
“Tumepoteza mechi mbili kwenye ligi hadi sasa na tupo nafasi ya nne kwenye msimamo, bado tunayo nafasi ya kurekebisha makosa, ukizingatia ligi ndiyo kwanza imeanza sioni kama tumefanya vibaya, ingawa ushindani ni mkubwa kwa timu nne za juu,” alisema Kiiza.
Pia mshambuliaji huyo alisema kuanza kwake vizuri kuitumikia klabu hiyo kumetokana na mashabiki wa timu hiyo kumuamini na kumpa ushirikiano wa kutosha tangu siku ya kwanza alipotua nchini kusaini mkataba wa kuichezea Simba.
Ushindani katika kuwani ufungaji bora msimu huu umekuwa mkubwa, ambapo mshambuliaji wa Stand United Elias Maguri, anaongoza mbio za ufungaji bora kwa sasa akifunga mabao tisa huku Ngoma na Hamisi Kiiza wa Simba wakiwa nafasi ya pili kila mmoja akiifungia timu yake mabao nane.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.