Polisi wakamata magunia ya dawa za kulevya mkoani Tanga



JESHI la Polisi mkoa wa Tanga linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kusafirisha kilo 462 za mirungi. Watuhumiwa hao ni dereva wa lori aina ya Fuso lenye namba za usajili T 860 BYQ, mkazi wa Kibaha Picha ya Ndege Alois na mkazi wa Mbauda mkoani Arusha, Rashid Juma (22).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zuberi Mwombeji akizungumza na waandishi wa habari alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Novemba 11 mwaka huu saa 11.45 alfajiri katika kijiji cha Kwamdulu, kata ya Kwamsisi wilayani Korogwe.
“Gari hilo lilikuwa likitokea mkoani Arusha kuelekea jijini Dar es Salaam likiwa na magunia 23 ya mirungi sawa na kilo 462 ilikuwa imechanganywa na maharage ili kuwazuga askari wasielewe kwamba ni mirungi lakini kutokana na uwezo wa jeshi la Polisi tumeweza kuwabaini,” alisema.
Katika tukio jingine, mkazi mmoja wa wilayani Mkinga, Shabani Aweso (35) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kusafirisha kilo 35 za mirungi. Kamanda Mwombeji alisema Aweso alikamatwa Novemba 11 mwaka huu akisafirisha mirungi hiyo kutoka mkoani Tanga kuelekea jijini Dodoma ndani ya basi la Kampuni ya Tashrif katika kizuizi cha polisi kilichopo eneo la Kabuku wilayani Handeni.
Alisema watuhumiwa wote wako mahabusu na uchunguzi unaendelea na utakapokamilika wahusika watafikishwa mahakamani.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.