Majambazi yapora kininja Sinza Kijiweni
WATU
wanaodaiwa kuwa ni majambazi wakiwa wameficha nyuso zao huku wakiwa
wamebeba silaha kali mkononi jana walilisimamisha eneo la Sinza
Kijiweni, jijini Dar es Salaam kwa takribani nusu saa baada ya kuvamia
gari lililokuwa limebeba pombe aina ya Banana na kupora Sh milioni 34.
Tukio
hilo ambalo liliambatana na milio ya risasi takribani sita zilizopigwa
hewani lilitokea saa 5:30 mchana katika makutano ya barabara ya
Shekilango na Tandale, Sinza Kijiweni.
Watu
walioshuhudia tukio hilo dakika chache kabla ya waandishi wa gazeti
hili hawajafika walieleza kuwa watu hao wanaodaiwa kuwa ni majambazi
walikuwa katika pikipiki tatu wakati wanalivamia lori hilo aina ya Fuso
lenye namba za usajiili T 210 BUU.
Inaelezwa
kuwa baada tu ya kulivamia walianza kwa kupiga risasi katika tairi la
kushoto hali iliyozua taharuki kwa watu waliokuwa karibu na eneo hilo
akiwemo mwandishi wa habari hizi.
Watu
hao ambao matendo yao yanaonyesha kuwa na utaalamu wa masuala ya silaha
na kudhibiti walijipanga kila mmoja akiwa na kazi yake.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, mmoja alionekana akilizuia gari hilo kwa mbele huku akiwa ameelekeza bunduki kwa dereva.
Mwingine alionekana upande wa ubavuni wa gari hilo akimwamuru dereva wake atoe begi walilodai kuwa na fedha hizo.
Taarifa
hizo zinadai kuwa katika kundi hilo, mtu mwingine wa tatu alikuwa
upande wa eneo la Sinza Madukani na yeye alipewa shughuli ya kuzuia
magari yanayoelekea katika eneo la tukio ambalo ni Sinza Kijiweni.
Inaelezwa kuwa wakati wakiwa katika harakati za kupora,
walipiga
risasi moja kwenye tairi la gari, risasi nyingine ilipigwa juu ili
kutisha na kutawanya watu waliokuwa karibu na eneo hilo, haikufahamika
mara moja risasi nyingine mfululizo kama tatu zilizopigwa hewani
zilitokea wapi.
Hali
hiyo ilizua taharuki si tu miongoni mwa raia waliokuwa karibu na eneo
hilo bali pia kwa watu hao wanaodaiwa kuwa ni majambazi na hivyo
kuwafanya wafyatue risasi nyingine kama mbili kuelekea upande ilipo
Benki ya BOA na Kituo cha mafuta cha Puma ambako mara nyingi kunakuwa na
ulinzi.
Hata
hivyo, watu hao walifanikiwa kuchukua begi lililokuwa na fedha na
wakati wakitokomea wakiwa kwenye pikipiki zao hizo aina ya boxer
mwandishi wa habari hizi aliwaona.
Baada
tu ya watu hao kuondoka umati mkubwa wa watu ulionekana kukimbia
kuelekea eneo la tukio tofauti na mwanzo ambapo walikimbia na
kusababisha vumbi kubwa.
Waandishi
wa MTANZANIA Jumamosi hata walipowafikia dereva pamoja na wasaidizi
wake wawili waliokuwamo katika lori hilo ili kujua chanzo cha kuvamiwa
kwao, walionekana kutetemeka kiasi cha kushindwa kujieleza.
Kila mmoja alionekana akipiga simu na hakuna aliyeweza kulizungumzia tukio hilo kwa ufasaha.
Baada
ya muda saa sita mchana gari ndogo ya polisi aina ya Ashok Leyland
yenye namba PT 2083 liliwasili katika eneo hilo ambapo askari watatu
walishuka huku wakiwa na silaha.
Kutokana
na kitendo cha askari hao kuchelewa kuwasili katika eneo la tukio
wananchi walionekana kuchukizwa na kitendo hicho huku mmoja akisikika
akisema: “Hawa askari wetu wanajua tu kuzuia maandamano,” alisema
shuhuda huyo.
Gazeti
hili liliwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni,
Camillius Wambura ambaye mara kadhaa majibu yake yalikuwa, “sina taarifa
nilikuwa msibani, nipigie baadaye.”
Alipopigiwa
baadaye alijibu; “bado sijalifanyia kazi suala lako subiri nitakupigia”
na mara ya tatu kabla gazeti hili halikwenda kiwandani alipopigiwa simu
hakupokea kabisa.
Eneo la Sinza mara kadhaa limekuwa likikumbwa na matukio ya utapeli, ujambazi na kupora kwa kutumia risasi.