MPYAAA>>>DARASA LA PILI KUFANYA MTIHANI WA TAIFA KUANZIA MWAKANI


BARAZA la Taifa la Mitihani (NECTA) limesema ili kutekeleza sera ya elimu ya mwaka 2014, watoto wataanza kukariri darasa kuanzia wakiwa darasa la pili. Alisema hatua hiyo itachukuliwa endapo watashindwa mtihani wa kujipima ambao utaanza rasmi mwakani kwa wanafunzi wa ngazi hiyo ya elimu. 


Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza na gazeti hili. Alisema kufanyika kwa mitihani hiyo kunakwenda sambamba na kuipa hadhi mitihani ya kupima wanafunzi katikati ya masomo ya darasa la nne na kidato cha pili ambayo kwa sasa itakuwa chini ya baraza hilo tofauti na ilivyokuwa awali. 

Dk. Msonde alisema kwa upande wa mitihani ya darasa la pili, matokeo ya mitihani hiyo itasaidia kuwatenga wanafunzi hao kwenye makundi matatu ambayo walimu watatakiwa kuyafanyia kazi kuhakikisha watoto hao wakiendelea na madarasa ya juu watafanya vizuri.

Alisema kwa kuwaandaa watoto kwa mitihani hiyo, anaamini mpaka wakiwa wanamaliza darasa la saba hakuna ambaye atakuwa hajapata stadi za kusoma na kuandika kama ilivyo kwa sasa ambako baadhi uhitimu elimu ya msingi wakiwa hawajui kusoma na kuandika. Kwa kuanza kuwapima wakiwa darasa la pili watakuwa wanaangalia kwenye stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu huku mitihani mingine kama ile ya darasa la nne ikipandishwa hadhi na kuwa chini ya baraza. Tunaamini suala la watoo kumaliza darasa la saba baadhi wakiwa hawajui kusoma na kuandika litaisha, alisema. 

Alisema mipango ya sera hiyo ikikamilika, mtihani wa darasa la saba ambao hivi sasa ni wa kuhitimu elimu ya msingi, utakuwa wa kupima kama ulivyo ule wa darasa la nne kwa sababu elimu ya msingi mwisho itakuwa kidato cha nne. Siwezi kusema ni lini hili litaanza kwa sababu utekelezaji wa sera ni mchakato, lazima kwanza madarasa ya sekondari yaongezwe. 

Mitaala ibadilike kama hivi sasa ambavyo ya darasa la kwanza na la pili imebadilika na ndiyo kwanza tunaanza kuwapima wanafunzi kwa mtihani huo wa darasa la pili. 

Faida nyingine ya mtihani huo na ule wa darasa la nne ni kuhakikisha mpaka mtoto anafika darasa la saba, wale watakaopata alama 100 chini ya 250 ambao kwa sasa ndiyo ufaulu wawe wameongezeka, alisema Dk. Msonde. Alisema ili kuona namna bora ya kuanza kufanya mtihani huo mwakani, leo watoto wa darasa la pili kutoka shule 66 zilizo kwenye mikoa 11 watafanya mtihani huo ikiwa ni sehemu ya majaribio.

Alisema kwenye mikoa hiyo zimechaguliwa wilaya ambazo zimetoa shule moja ya kijijini, moja ya mjini na nyingine ya mchepuo wa Kiingereza.

Chanzo: Mtanzania







Theme images by hanoded. Powered by Blogger.