MKE WA LOWASSA AKATAA UBUNGE
Mke wa aliyekuwa Mgombea Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Mama Regina Lowassa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilitangaza mgawanyo wa viti maalum
jana ulioonyesha kuwa Chadema imevuna viti 36, ikiwa ni ongezeko kubwa
lililotokana na kufanya vizuri zaidi katika majimbo kulinganisha na
uchaguzi wa mwaka 2010 wakati walipopata idadi ya viti maalum
isiyokaribia 30.
Taarifa iliyopatikana jijini Dar es Salaam jana ilieleza kuwa mama
Lowassa ambaye alifanya kazi kubwa ya kupigania mafanikio ya Chadema
wakati wa kampeni, ameikataa kwa nia njema nafasi hiyo aliyopewa na
kamati Kuu ya Chadema.
Ilielezwa kuwa Mama Regina aliipokea kwa heshima nafasi hiyo,
lakini anaamini bado anao uwezo wa kushughulikia matatizo ya akina mama
na watoto akiwa nje ya bunge.
"Naishukuru kamati kuu ya chama changu kwa heshima hii kubwa
waliyonipa na ninaithamini sana. Lakini naamini nitaendeleza mapambano
ya kuwaletea kina mama mabadiliko na kwa ufanisi zaidi nikiwa nje ya
bunge," Mama Lowassa alikaririwa akisema.
Kamati Kuu ya Chadema iliamua kumtunuku nafasi ya ubunge viti
maalum kutokana na mchango mkubwa alioutoa wakati wa kampeni ambao kwa
kiasi kikubwa ulisaidia upatikanaji wa kura nyingi kwenye majimbo ya
uchaguzi na mwishowe chama hicho kikatangaziwa na NEC kupata nafasi 36
za viti maalum.
CHANZO:
NIPASHE