MH. LOWASSA KUTOA TAMKO ZITO LEO HUKO ARUSHA
Aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema, Edward Lowassa anatarajia kuhutubia mkutano wa kumnadi mgombea wa ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema na kuwashukuru Watanzania kwa kura walizompa katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Jeshi
la Polisi limeridhia mkutano huo utakaofanyika viwanja vya Shule ya
Msingi Ngarenaro, lakini limepiga marufuku maandamano yoyote.
Huu
utakuwa mkutano wa kwanza wa hadhara kwa Lowassa tangu matokeo ya
uchaguzi mkuu yalipotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambayo
yalimpa ushindi mgombea wa CCM, Dk John Magufuli. Lowassa alipata kura
6,072,848, sawa na asilimia 39.97 wakati mshindi Dk Magufuli
alijikusanyia kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46
“Tunatarajia
kesho (leo) aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema chini ya mwavuli wa
Ukawa, Edward Lowassa atahutubia mkutano wa kampeni wa kawaida
akiongozana na viongozi wengine wa kitaifa,” alisema Katibu wa Chadema
Wilaya ya Arusha, Lewis Kopwe, alipozungumzia kukamilika kwa maandalizi
yote ya mkutano huo jana.
Kopwe
alisema mkutano huo ni sehemu ya mikutano ya kampeni za uchaguzi mdogo
wa Jimbo la Arusha Mjini na amehimiza amani na utulivu vitamalaki katika
mkutano huo.
Kamanda
wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas jana alisema wamepiga marufuku
maandamano ya aina yoyote katika mikutano ya kampeni inayoendelea.
Alionya
Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote ambaye
ataandamana na kusababisha kuvunjika kwa amani katika Jiji la Arusha.
“Kuna watu, kwa maslahi yao, wanataka kutuvunjia amani, sasa tunaonya
tutachukua hatua kali kwa yeyote ambaye atavunja sharia,” alisema
Kamanda Sabas.
Pamoja
na onyo hilo, alisema kuwa hadi jana jeshi hilo, lilikuwa halijapata
barua yoyote ya kutaka maandamano na hata ikiwapo hawatakuwa tayari
kuruhusu yafanyike. Pia, alisema jeshi hilo liko vizuri na limejipanga
kuhakikisha amani na utulivu vinadumu kama ilivyokuwa wakati wa Uchaguzi
Mkuu Oktoba 25 mwaka huu.
Katika
hali inayoonyesha kwamba Jeshi la Polisi halitanii, jana jiji la Arusha
lilikumbwa na taharuki kutokana na magari makubwa ya kurusha maji ya
kuwashwa kupitishwa mitaani huku yakiwa kwenye mwendo kasi.
Kamanda
Sabas alisema kilichokuwa kinafanyika ni mazoezi ya kawaida ambayo
yanathibitisha kuwa polisi ipo imara. “Haya ni mazoezi ya kawaida,
tunajua uchaguzi bado unaendelea na tumejipanga kulinda amani ya
Arusha,” alisema.
Lema,
ambaye anajiandaa kutetea kiti hicho alisema kwenye mkutano wa uzinduzi
wa kampeni kwamba Lowassa atazungumza leo na Watanzania, pia
kuwashukuru kwa kumpigia kura nyingi.
Naye
Mbunge mteule wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi “Sugu” alisema katika
mkutano huo Chadema watatoa tamko zito la kwanza mara baada ya uchaguzi
huo wa madiwani, wabunge na rais kumalizika.