'Mchagueni Lema tukapiganie Tume Huru ya Uchaguzi'
Mbunge mteule wa Jimbo la Monduli, Julius Kalanga.
Kalanga aliyasema hayo juzi katika mkutano wa ufunguzi wa kampeni za mgombea huyo uliofanyika eneo la Soko Kuu jijini hapa.
“Arusha msifanye makosa, mchagueni Lema tukapiganie Katiba bora ya Tanzania na Tume Huru ya Uchaguzi,” alisema na kuongeza:
“Tusiwe wanyonge watu wa Arusha, unachukuaje kura ya Chadema na
kuwapa watu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili watoto wako wafe njaa,
hata kama anayegombea CCM ni shemeji yako usimpe kura yako,” alisema.
“Haiwezekani mkawapigia kura madiwani 24 wa Chadema dhidi ya mmoja
wa CCM jimboni hapa, halafu mkashindwa kumpigia kura mgombea ubunge wa
chama chenu,” alisema.
Aidha, alikemea tabia ya baadhi ya wakazi wa hapa kujiandaa kupiga
kura kwa misingi ya ukabila akisema uchaguzi wa mbunge utakaofanyika
Desemba 13, mwaka huu sio wa kumchagua kiongozi wa kimila.
“Hatuchaguzi kiongozi wa mila hapa, tuwakatae wanaofanya ubaguzi,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge mteule wa Jimbo la Simanjiro, James Ole
Millya (Chadema), alimtaka Rais Dk. John Magufuli kujenga mfumo wa
kutatua ufumbuzi wa kero za wananchi badala ya yeye kupita kila kona
kukagua shughuli za utendaji.
“Magufuli ameanza kwa kufukuza huyu na kumsimamisha yule…tunataka
akae ofisini na kujenga mfumo mzuri wa utendaji serikalini. Hawezi
kutembelea kila sehemu mwenyewe,” alisema.
Aliwapongeza watu wa mikoa ya Kaskazini kwa kutochezea kura zao kama ilivyokuwa maeneo mengine.
Alisema uchaguzi mkuu uliopita uliandaliwa kwa muda mrefu kuwezesha
wagombea wa CCM kushinda, hivyo kuufanya kuwa kiini macho. Akizungumza
katika mkutano huo, Lema alisema hatakubali kuibiwa kura zake na kupewa
mgombea mwingine.
“Wamenyang’anywa ubunge wagombea wengi wa Chadema, lakini mimi sitakubali kudhulumiwa hilo kabisa,” alisema.
Aidha, alitoa angalizo kwa polisi mkoani hapa kutenda haki, badala ya kufanya kazi za ukada wa CCM.
Alisema kumekuwa na tabia ya polisi kujiingiza katika masuala ya siasa huku akidai kuwa wamekuwa wakitoa upendeleo kwa CCM.
CHANZO:
NIPASHE