MAZUNGUMZO YA SHEIN NA SEIF YAKO HAPA>>>>SOMA KUJUA ZAIDI MAKUBALIANO YAO
WANANCHI wengi Zanzibar wamefurahishwa na juhudi zilizoanza kuchukuliwa za mazungumzo kati ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad ambayo yameshusha joto la kisiasa Zanzibar lililotokana na kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Katika mazungumzo na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana mjini hapa, baadhi ya wananchi walisema kwamba hatua hiyo itarudisha mazingira ya kawaida kwa wananchi na pia kupunguza mfumuko wa bei ambao ulianza kushika kasi katika bidhaa mbalimbali.
Mkazi wa Makadara, Ali Haji, aliwapongeza viongozi hao ambao walikuwa wagombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu kupitia vyama vyenye wafuasi wengi vya CCM na CUF.
Haji alisema mazungumzo yaliyoanza kufanywa na viongozi hao kwa kiasi kikubwa yatapunguza joto la kisiasa lililopo hapa lililochangiwa kwa kiasi kikubwa na kufutwa kwa uchaguzi huo na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Mfanyabiashara wa Soko Kuu la Mwanakwerekwe mjini Unguja, Hamad Said, alisema uamuzi uliochukuliwa na viongozi hao unastahili kupongezwa kwa sababu utarudisha mazingira ya kawaida ya wananchi kufanya kazi zao za kila siku ambazo zimedorora kwa muda wa wiki mbili sasa.
Said alisema wameshindwa kufanya biashara vizuri katika soko hilo kwa sasa kwa sababu mbalimbali, ikiwemo bidhaa kushindwa kuingia nchini kutoka Tanzania Bara. Alisema hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa bidhaa nyingi muhimu bei yake kupanda juu na kuwapa wakati mgumu wananchi wenye kipato cha chini.
“Wafanyabiashara tumefurahishwa na hatua zilizochukuliwa na viongozi wetu wakuu wa kuanzisha mazungumzo ambayo lengo lake ni kuondosha hali ya wasiwasi iliyopo sasa ambayo athari zake zimeanza kujitokeza ikiwemo ugumu wa maisha ya wananchi wa kawaida,” alisema Said.
Mgombea wa urais wa Zanzibar kwa chama cha AFP, Said Soud ameitaka ZEC kutangaza siku ya kurudiwa kwa uchaguzi mwingine ili wananchi watumie nafasi yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi wanaowataka.
Akizungumza na gazeti hili kutoka Pemba, Soud alisema ZEC haitakiwi tena kukaa kimya mara baada ya kufutwa kwa uchaguzi huo kwani kufanya hivyo ni kuweka mazingira magumu ya kisiasa nchini.
Hali ya kisiasa Zanzibar imezorota mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 ambao ulifutwa na ZEC kwa maelezo ya kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria za uchaguzi. Juzi, Dk Shein na Maalim Seif walikutana katika Ikulu ya Zanzibar katika kile kinachoaminika ni kusaka suluhu ya mgogoro ulioibuka baada ya uamuzi wa ZEC. Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa baada ya mazungumzo yao.