Kikwete ateta saa moja na Maalim Seif

RAIS Jakaya Kikwete jana alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama cha Civic United Front (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, Ikulu jijini Dar es Salaam. Maalim Seif pia alikuwa mgombea urais wa Zanzibar wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu uliofanyika Oktoba 25, lakini ukafutwa siku tatu baadaye na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, viongozi hao wawili walikutana kwa kiasi cha saa moja Ikulu, kuzungumzia hali ya kisiasa Zanzibar kufuatia ombi la Maalim Seif kutaka kukutana na kuzungumza na Rais Kikwete.
“Viongozi hao wamekubaliana kuwa mashauriano yaendelee kufanyika baina ya pande zote zinazohusika na hali ya kisiasa Zanzibar,” ilieleza taarifa ya Ikulu. Wakati viongozi hao wakikutana Dar es Salaam, vyama vinne vya siasa vilivyoshiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, vimeungana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuunga mkono tamko la kufutwa kwa uchaguzi huo.
Tamko hilo limetolewa na kusainiwa na viongozi wa vyama vya siasa waliogombea urais wa Zanzibar, ambao ni CCK, TLP, SAU na AFP, ambao wameitaka ZEC ikiwemo wajumbe wake kuwajibika kwa sababu ya kushindwa kusimamia uchaguzi huo.
Tamko hilo lililosainiwa kwa pamoja, limesema kitendo cha ZEC chini ya Mwenyekiti wake Jecha Salum Jecha kushindwa kusimamia uchaguzi huo, kimetishia nchi na kutaka kuiingiza katika fujo na vurugu za kisiasa.
Aidha, tamko hilo limeitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wote wa Tume, ambao kwa njia moja au nyingine wamevuruga kazi hiyo na kuitia nchi katika hasara kubwa.
“Sisi viongozi wa vyama vya siasa tulioshiriki Uchaguzi Mkuu tunatoa tamko la kutaka watendaji wa Tume kuwajibishwa kwa kuzembea na kuharibu Uchaguzi Mkuu na kutaka kuiingiza nchi katika gharika,” walieleza viongozi hao.
Aidha, katika tamko hilo, viongozi wa vyama vya siasa wamemtaka Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kumfuta kazi Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad kutokana na kupoteza sifa za uongozi.
Tamko hilo lilisema Maalim Seif alijitangazia ushindi mapema, kinyume cha sheria za Tume ya Uchaguzi na hivyo kuzua hofu na wasiwasi na ndiyo chanzo cha kuvurugika kwa uchaguzi huo.
Viongozi wa vyama vya siasa waliotia saini tamko hilo ni mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCK, Ali Khatib, Hafidh Hassan Suleiman wa TLP, Issa Mohamed Zonga wa SAU na Said Soud Said wa AFP Wakulima.
CCM ilikuwa ya kwanza kupinga Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 na kukubaliana na ZEC kufutwa kwake. Sababu zilizotolewa na CCM kupitia msemaji wake, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai ni pamoja na mawakala wa chama hicho wa Pemba kuzuiliwa kuingia katika vituo vya kupiga kura bila ya sababu za msingi.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.