Chanzo Kikubwa Cha Mabadiliko Ya Maisha Yako, Kinaanzia Hapa.
Inawezekana
ukawa ni miongoni mwa aina ya watu ambao wamekuwa wakijiuliza maswali
mengi sana kuhusu sababu ya baadhi ya vitu kama vile hali ngumu za
kimaisha, matatizo anayokabiliana nayo binadamu kila siku na shida
zinginezo za maisha haya.
Pia najua umekuwa una maswali kama ‘Kwa
nini mimi? Nitakuja kuwa nani? Nitafanya nini na maisha yangu? Malengo
yangu ni nini? Je, ndoto zangu zinaweza kutimia? Naweza kufanya mambo
makubwa na kuwa na pesa.’ Yote hayo yamekuwa maswali yanayosumbua vichwa vya watu wengi.
Tambua
kwamba, akili yako ndiyo chanzo kikuu ambacho huweza kuweka mabadiliko
katika maisha yako. Hivyo, basi kama tungekuwa hatuna akili ya
kujitawala na kutawala ,maisha yasingekuwa na maana. Maisha ya mafanikio
kamili ni matokeo ya akili imara yenye mawazo sahihi.
Pamoja
na maswali yote hayo ambayo umekuwa ukijiuliza umekuwa huna uhakika je,
kweli majibu hayo yapo? Na kutokana na kukosa majibu hayo umekuwa mara
nyingi ukikata tamaa na kuona maisha yako tena basi hayawezekani kwa
lolote.
Lakini
ninachotaka kukwambia unao uwezo mkubwa wa kubadili maisha yako ikiwa
utaamua kutumia uwezo wa akili ulionao kikamilifu. Kumbuka akili yako,
ndicho chanzo kikuu cha mabadiliko. Na utaweza tu kufanikiwa kwa urahisi
kwa kufanya mambo haya:-
1. Kuwa kiongozi na mlinzi wa akili yako.
Kumbuka
siku zote maisha yako yote yapo mikononi mwako. Ili kufanikiwa
inahitajika akili yako kwanza iweze kujiandaa, kupanga, kukubali na
kuamini kwamba maisha bora ni yako na si vinginevyo. Akili uliyonayo
ndiyo hazina pekee kwa maisha yenye mafanikio makubwa.
Kwa
namna yoyote ile ukishindwa kuwa kiongozi wa akili yako kuilekeza
kwenye mafanikio makubwa ambayo ni haki yako kuyapata, mafanikio hayo
utaishia kuyaona kwa watu wengine tu basi. Utajitahidi kwa hili mara
lile lakini kwa sababu umejifunga itakuwa ngumu kwako kufanikiwa.
Watu
wengi wameshindwa kuwa walinzi wa akili zao na kuelekea kwenye njia ya
mafanikio. Matokeo yake wamefungwa na mawazo potofu kama ‘ Sina nyota, sina kipaji, sina uwezo wa kutosha kufanya jambo hili’na mambo mengineyo mengi ambayo umekuwa ukijisemea na ndiyo chanzo cha umaskini maishani mwako.
MABADILIKO YOTE YANAANZIA NA AKILI. |
2. Jijengee fikra huru.
Kama
utaendelea kuzifunga fikra zako ni wazi utaendelea kubaki na matatizo
yako hayo. Umefika wakati wa kuziachia fikra zako na kuwa huru ili
kushinda matatizo yote unayokabiliana nayo. Jiambie mwenyewe ‘Sijazaliwa kwa ajili ya matatizo, nimezaliwa kuwa na mafanikio’
Hakuna
namna unavyoweza kutatua na kuondoa shida na matatizo yako bila ya
akili yako kuitumia kikamilifu. Hauhitaji hatua ya kufikia kukata tamaa
na kujiingiza kwenye ulevi wa pombe. Suluhisho pekee ulilonalo ni
kuitumia akili yako kikamilifu na kwa makini.
Umefika
wakati wa kujenga picha mpya ya mafanikio na kuondoa kujiwekea vikomo
vya viwango vya kimafanikio. Utafanikiwa hili kwa kujiwekea fikra huru
ambazo zitakusaidia kutatua matatizo uliyonayo. Kwani ikumbukwe chanzo
chote cha mafanikio na mabadiliko kinaanzia kwenye akili yako.
Haijalishi
kwamba upo kwenye matatizo mengi kiasi gani. Haijalishi umeumizwa mara
ngapi na maisha. Kwa vyovyote vile wewe ni mshindi wa maisha yako ikiwa
utaamua kuwa kiongozi na mlinzi wa fikra zako pamoja na kujijengea
fikra huru zitakazokupa maisha ya mafanikio siku hadi siku.
Kwa makala nyingine nzuri karibu kwenye DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Simu; 0713 048 035,