KAMA ULIKUA HAUJUI HAWA NDIYO MABILIONEA WASIO NA HURUMA







PADRI Silvanio na Sista Mariastela wamewachenga polisi uwanja wa ndege na kupanda gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili TZL 203 ABO, polisi wanalifuatilia gari hilo kutokea Kibaha na wengine wanatokea Chalinze kuelekea Kibaha, wanaamini lazima watakutana nao mahali fulani katikati na kuwakamata watawa hao.

Cha kushangaza walilikuta gari hilo likiteketea kwa moto kando ya barabara, wakaangalia namba na kujiridhisha kabisa ndilo walilokuwa wakilifuatilia! Je, Padri Silvanio na Sista Mariastela wameteketea ndani ya moto huo?SONGA NAYO…

ASKARI wa Kibaha ndiyo walikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio, wakifuatiwa na askari wa Chalinze, wote wakashuhudia gari aina ya Toyota Corolla lenye namba TZL 203 ABO likiteketea mbele ya macho yao, hawakuwa na la kufanya zaidi ya kusubiri moto upungue ili waweze kuangalia kama Padri Silvanio na Sista Mariastela walikuwa wameteketea ndani ya moto huo.

Hapakuwa na gari la zimamoto ambalo lingeweza kufanya kazi ya kuuzima moto huo, ikabidi wote watulie mpaka moto ulipopungua wenyewe, wakaanza kuuzima kwa matawi ya miti na mchanga! Walipochungulia ndani hapakuwemo na Padri Silvanio na Sista Mariastela!

“Wako wapi?” Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Pwani Lameck Mgumile aliuliza akionyesha mshangao wa wazi.
“Inawezekana wamechoma gari halafu wakatoroka.”
“Lakini namba za gari ni hizihizi!”
“Ndizo tulizopewa, TZL 203 ABO!”

“Basi inawezekana kweli wametoroka, lakini kwa nini watawa ambao jamii yote inawaamini wafanye kitendo hiki? Nini kimejificha nyuma yao, lazima kuna jambo kubwa sana!”

“Kweli kabisa, hebu fikiria, wameuza kila kitu wakaelekea uwanja wa ndege ambapo ndege waliyotakiwa kuipanda hawakuipanda, wakatoroka kwa gari ambalo mbele ya safari wamelichoma, hawa siyo watawa wa kawaida, lazima ni watu hatari sana.”
“Sasa tunafanyaje?”

“Acha tumpigie Kamanda wa Polisi wa Mkoa, awasiliane na watu wa Interpol kuwajulisha juu ya kilichotokea, tupate maelekezo mengine!”

Simu ilipokatwa, haraka sana ikapigwa kwa Kamanda wa Polisi ambaye alielezwa tukio zima naye baaada ya kusikiliza hadi mwisho akakata simu na kupiga Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na kuwataarifu juu ya kilichotokea, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hussein Rajabu akapewa taarifa hizo na kuchanganyikiwa kabisa, mpelelelezi Denis Crapton alionekana kutoamini kilichotokea.

“Haiwezekani hawa watu wakawa wajanja kiasi hiki, nahisi tunapambana na mtandao mkubwa sana uliojiandaa kuhakikisha hawakamatwi, ninapofikiria hata namna walivyotoroka uwanja wa ndege nashindwa kuelewa, gari walilipata wapi, waliwezaje kupita upande wa VIP bila kuhojiwa? Tunahangaika na mfumo lakini ni lazima tuwakamate, ipo siku nitawatia mkononi na kufahamu ni akina nani hasa hawa Padri Silvanio na Sista Mariastela wakati watawa hao wote wawili walishakufa na kufukiwa kisimani,” Denis Crapton aliongea kwa uchungu.

Bila kupoteza wakati Kamishna Msaidizi Hussein Rajabu alipiga simu polisi Kibaha na kuwashauri wachukue askari wa mbwa ambao mara tu baada ya kufika eneo la tukio lazima wangeelekeza njia ambayo Padri Silvanio na Sista Mariastela waliipitia kwa kunusa pua zao chini, wazo hilo lilikubaliwa na gari la polisi lenye mbwa wawili wataalamu wa kunusa likaondoka Kibaha kwa kasi mpaka eneo la tukio.

Mbwa waliposhushwa na kuelekeza pua zao ardhini walianza kutembea kuingia vichakani wakiendelea kunusa, askari wakiwa nyuma yao, bunduki mkononi zikiwa tayari kwa lolote.

Mbwa hawakukoma kunusa, wala kuonyesha kuchoka, kutwa nzima mpaka jua linazama walikuwa bado wakiendelea na safari huku pua zao zikiwa zimeelekezwa ardhini, dalili kwamba watu waliokuwa wakiwafuatilia walikuwa mbele, askari walikubaliana kuendelea na kazi hiyo usiku kucha wakipita katikati ya mapori, matumaini yao yakiwa ni lazima wangewakuta Padri Silvanio na Sista Mariastela mahali fulani wakiwa wamechoka na kulala.

Mpaka kunakucha asubuhi walikuwa bado hawajawafikia, kundi la askari zaidi ya thelathini wenye bunduki aina ya SMG walikuwa wamechoka kabisa, wakiendelea kuwafuatilia mbwa kwa nyuma. Njaa pia ilikuwa ikiwasumbua lakini ilibidi wavumilie, kazi waliyopewa ilikuwa ni kuwasaka watawa hao, ambao wakati huo hawakutafsirika kama watawa tena, bali magaidi.
***
Padri Silvanio na Sista Mariastela walikuwa wamechoka hoi bin taaban, miguu ilikuwa imevimba na kuchanika, miili yao imechanwa na miiba kwa sababu ya kupita vichakani! Hawakujisikia kuendelea tena, ikiwa tayari ni saa tisa alasiri, wakaamua kuingia ndani ya kichaka na kujilaza, Padri Silvanio akitafakari mahangaiko waliyokuwa wakiyapata sababu ya utajiri.

“Vanessa!” akaita katika majina yao halisi.
“Abe! Jina hilo nilishalisahau kabisa, nimezoea watu wanaponiita Sista Mariastela,” mwenzake akaitikia na kujieleza.

“Nimechoka, tumeteseka sana sababu ya tamaa ya utajiri, juhudi zangu zote naona zimekaribia kufika mwisho, sina uhakika kama naweza kuendelea tena kujificha baada ya hapa, nikikamatwa safari hii nitakuwa radhi kwa lolote!”
“Unakata tamaa upesi!”
“Upesi?”
“Ndiyo!”

“Hii siyo upesi, nimeteseka mno, sasa niko tayari kufa na kwa kweli dunia nzima inafahamu kwamba sisi ni wafu, hivyo tukifa sasa hivi itakuwa ni kama tunakufa mara ya pili!”

Vanessa akafumba macho na kujaribu kutafakari walikotokea, mambo yote waliyoyafanya kama wanawake, yeye mwenyewe moyoni mwake akakiri kabisa dunia ilikuwa na haki ya kuwaita wanawake hatari waliohangaisha majeshi ya polisi kuliko mhalifu mwingine yeyote katika historia ya dunia, akili yake ikamrudisha kwenye kufikiria namna walivyoweza kukitoroka kifo cha kudungwa sindano ya sumu.
“Hivi Yousef Emmanuel yuko wapi?” Vanessa aliuliza.

“Tangu mara ya mwisho tulipoonana naye gerezani Gontwa sijawahi kusikia habari zake!”
“Malipo yake alipata?”
“Alipata.”

“Lazima atakuwa kwenye matatizo mahali fulani, yawezekana hata aliuawa, mtu huyo ni wa muhimu sana katika maisha yetu, ni bora hata kama tukidungwa sindano ya sumu tumuachie yeye utajiri wetu.”
“Ni kweli kabisa.”

Yousef Emmanuel alikuwa ni raia wa Israel aliyekuwa na kampuni yake binafsi iliyoitwa Mastermind International, makao yake makuu yakiwa nchini Israel katika Jiji la Tel Aviv. Mtu huyu alikuwa ni mwenye akili nyingi kupindukia, alizaliwa na kipaji na karama ya ajabu, akasoma mpaka kufikia ngazi ya uprofesa ndani ya miaka ishirini na tano, dunia nzima ikamtangaza kama profesa mwenye umri mdogo kuliko mwingine yeyote duniani.

Wakati alihitajika na mataifa makubwa kama Marekani na Urusi ili akafanye kazi katika kutengeneza mitambo ya nyuklia, Yousef alikataa ingawa malipo yalikuwa ni makubwa mno, akaamua kujiajiri mwenyewe kwa kuanzisha kampuni yake binafsi ya Mastermind International.

Alichokifanya na kampuni yake ni kusaidia mataifa mbalimbali duniani kutatua matatizo yaliyowasumbua, hata matajiri wakubwa waliohitaji suluhisho kwa matatizo yaliyokwamisha shughuli zao! Kampuni yake ilikuwa ni ya kutoa majibu kwa matatizo yaliyoshindikana, akawa analipwa kiasi kikubwa cha fedha kuliko ambazo angelipwa kama angekubali kuajiriwa, ndani ya muda mfupi Yousef akawa tajiri.

Kampuni yake ilisaidia viongozi wengi duniani kuingia madarakani kwa kutengeneza program za kompyuta zilizoingilia kumbukumbu za tume za uchaguzi na kubadilisha matokeo bila viongozi wa tume kuelewa kilichoendelea, alikuwa na uwezo wa kuingia katika simu ya mtu yeyote na kujua alikuwa akiwasiliana na nani na waliongea nini.

Huyo ndiye alikuwa Yousef Emmanuel, ambaye baadaye alisikia juu ya Dk. Viola na Vanessa, mabilionea waliokuwa gerezani wakikabiliwa na kesi za mauaji, akasafiri kutoka Tel Aviv hadi Dar es Salaam na kukutana nao, akiahidi kuwasaidia kukiepuka kitanzi kama wakili wao Denis Crapton angeshindwa kuwatetea katika kesi iliyokuwa ikiwakabili.

“Utafanyaje?” Walimuuliza wakiwa ndani ya Gereza la Gontwa.
“Nyie hiyo niachieni mimi, jibu ninalo, muwe tayari kunilipa tu!”
“Malipo yako ni kiasi gani?”
“Dola milioni tano.”

“Tunakulipa sasa au mwisho wa kazi?”
“Nusu kabla ya kuanza kazi.”
“Tutaaminije kwamba kweli utafanya mambo unayosema?”
“Naomba mniamini.”

Ni Yousef Emmanuel aliyetafuta maiti za watu kutoka katika hospitali moja maarufu jijini Dar es Salaam na kuziingiza kwa siri ndani ya Gereza la Gontwa siku ya kudungwa sindani kwa Dk. Viola na Vanessa, akiwa amemhonga karibu kila mtu ili zoezi hilo lifanikiwe.

Akahakikisha umeme unakatika ghafla gerezani wakati Dk. Viola na Vanessa wamelala juu ya vitanda vya mauti, miili iliyovishwa sura zao za bandia ikapandishwa juu ya vitanda hivyo kwa kasi, umeme ukawaka na zoezi la kudunga sindano za sumu likaendelea bila watu waliokuwa wakifurahia vifo vyao kujua kuwa Dk. Viola na Vanessa waliondolewa gerezani wakiwa na sura za Padri Silvanio na Sista Mariastela.

Vanessa alikuwa amezama katika mawazo ghafla wakiwa wamelala chini ndani ya kichaka, ghafla akashituliwa na sauti za mbwa wakibweka nje ya kichaka hicho, alipochungulia aliona kundi kubwa la askari wakiwa wamesimama na bunduki mkononi.

“Viola, Viola, Viola!” alimuita nduguye aliyekuwa usingizini.
“Vipi?”
“Tumeingia mikononi mwao!”
“Kina nani?”
“Polisi!”
Miili ikawatetemeka, wakahisi haja ndogo zikipenya kwenye nguo zao za ndani.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.







Theme images by hanoded. Powered by Blogger.