Wabunge wachangia bajeti huku wakitangaza nia, wajue majina yao hapa
WABUNGE wa majimbo na viti maalumu wamechangia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2015/16, kwa kutangaza nia za kugombea ubunge.
Hadi
kufikia jana zaidi ya wabunge 20 kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
upinzani wa kuchaguliwa na viti maalumu walitumia mjadala huo kutangaza
nia.
Kangi Lugola
Mbunge
wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) akichangia juzi pamoja na kuingia
bungeni na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nje, aliweka bayana kuwa
Mwibara bila Kangi mwana wa Lugola haiwezekani.
Lugola
aliwataka wapigakura wake kutambua kuwa mafanikio ya huduma za kijamii
kama maji, umeme, afya, barabara na zingine zimepatikana kupitia yeye,
kwani miaka 55 ya uhuru hakukuwa na huduma hiyo.
Deo Filikunjombe
Mbunge
wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alisema miaka minne na nusu ambayo
amewewatumikia wananchi wa Ludewa amefanya vizuri, hivyo anatarajia
kurejea kuwaomba wamchague tena ili kukamilisha matarajio yao.
Filikunjombe
alisema wakati akichukua jimbo hilo kulikuwa na vijiji vitatu pekee
ndivyo vyenye umeme, lakini hadi kufikia leo vijiji 67 kati ya 77 vina
umeme ikiwamo huduma ya miundombinu.
Ester Matiko
Kwa
upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko (Chadema), aliweka
bayana kuwa anatarajia kugombea Jimbo la Tarime kupitia chama chake
iwapo kitampitisha ili aweze kuwajibika moja kwa moja kwa wananchi wake.
Matiko
alisema mbunge aliyekuwepo wa CCM, Nyambari Nyangwine ameshindwa
kutekeleza mahitaji ya wananchi hivyo ni vema waweze kumpima kupitia
Bunge kama anastahili kuwatumikia.
Ridhiwani Kikwete
Mbunge
wa Chalinze, Ridhwan Kikwete (CCM), alisema kuwa anatarajia kurejea
jimboni kuwaomba wananchi wamchague ili aweze kukamilisha mambo ambayo
yamebakia.
“Mheshimiwa
Mwenyekiti napenda kuwaambia wapigakura wangu wa Chalinze mchango huu
kwani ni wa mwisho kwa Bunge hili ila natarajia kurudi tena kuwaomba
niendelee kuwatumikia, kwani bado kuna mambo ambayo yamebakia
hatujayatekeleza,” alisema Ridhiwani.
Akichangia bajeti hiyo alisema CCM ndiyo chama pekee ambacho kimeweza kuwafikisha Watanzania katika hali ya sasa ya mafanikio.
Ridhiwani
alisema kumekuwa na sera ya afya kwa walemavu ya kutibiwa bure, lakini
bado hawapati huduma hiyo. Pia, alioomba Serikali kuangalia uwezekano wa
kujenga Hospital ya Chalinze ili iweze kusaidia kutoa huduma kwa wakazi
wa jimbo hilo.
Ester Bulaya
Kwa
upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM) ametangaza
rasmi kugombea Jimbo la Bunda na kusema waliosema amepooza si kweli ni
mzima wa afya.
Bulaya alisema alikuwa akiumwa, lakini kukawa na uvumi kuwa amepooza jambo ambalo si la kweli na kwa sasa ni mzima wa afya.
“Nimepona
na nitasimama kugombea ubunge Jimbo la Bunda, maombi yenu yamefanya
kazi na sasa nipo tayari kugombea,” alisema Bulaya.
Akichangia
bajeti hiyo, mbunge huyo alisema kumekuwa na matumizi makubwa ya dola
za Marekani hapa nchini kuliko shilingi ya Tanzania.
Bulaya
alisema hivi sasa baadhi ya Watanzania wanajivunia kutumia dola katika
kuwalipia watoto wao shule na hata katika malipo mbalimbali katika
hoteli.
“Miaka
ya nyuma akinamama wajasiriamali waliokuwa wakienda China kununua
bidhaa mbalimbali wakiwa na dola walikuwa wakija na mizigo ya kutosha,
lakini hivi sasa hakuna.
“Hivi
sasa kila ukitembea hatua moja mbili unakutana na duka la kuuza fedha
za kigeni hivi kweli uchumi wetu utapanda kupitia shilingi yetu lazima
kufanya jambo hapa,” alisema.
Amina Mwidau
Mbunge
wa Viti Maalumu, Amina Mwidau (CUF), alisema anatarajia kugombea Jimbo
la Pangani, kwani kila dalili za kushinda zipo na uwezo aliounesha
katika bunge hili ni sababu ya kushinda.
Mwidau
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za
Serikali (PAC), alisema wananchi wa Pangani wanahitaji mabadiliko ambapo
CCM haiwezi kuyaleta tena.
“Napenda
kutumia nafasi hii kueleza kuwa naenda kuchukua fomu kupitia CUF,
kwenda kukomboa Jimbo la Pangani na huo ndio mwendo wa Ukawa,” alisema.
Kuhusu
bajeti, alisema kitendo cha kuongeza tozo kwenye mafuta ya taa, diseli
na petroli ni aibu kwa Serikali kwani wananchi wa vijijini ndio wataumia
zaidi.
Mbunge
huyo alisema kila kona ya bahari ya Tanzania kuna bandari feki ambazo
zinaingiza mizigo kwa njia ya magendo, hivyo kukosesha Serikali mapato.
John Lwanji
Kwa
upande wake, Mbunge wa Manyoni Magharibi, John Lwanji (CCM), alisema
miaka 10 ambayo amekuwa mwakilishi wao imekuwa ya mafanikio na kwamba
atarejea kuwaomba wampe nafasi tena ya kukamilisha yaliyobakia.
Lwanji
alisema kwa kipindi hicho Manyoni Magharibi, ilikuwa iko nyuma
kimaendeleo kwa miaka mingi ila uwepo wake kumekuwa wa mafanikio makubwa
ya kuwepo kwa miradi ya maji, umeme, barabara na huduma zingine za
msingi.
Abdul Aziz Abood
Kwa
upande wake, Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdul Azizi Abood (CCM), aliweka
bayana kuwa anatarajia kurejea kwa wananchi wa Morogoro kuwaomba tena
nafasi hiyo kupitia CCM, kwani ameweza kutekeleza ilani ya chama
kikamilifu.
Alisema
jitihada zionazofanywa na Ukawa haziwezi kufanya lolote katika jimbo
hilo, kwani aliyoyafanya yanaonekana na kuahidi kuwa watashinda kwa
kishindo.
Kuhusu
bajeti aliitaka Serikali kujikita katika kuhakikisha kuwa viwanda
vinafanya kazi, kwani bila kuwepo kwa viwanda ni dhahiri kuwa uchumi
utashuka na shilingi.
Alitolea
mfano viwanda vya mafuta ambapo alisema kuwa pamoja na juhudi za
wakulima nchini kulima mazao ya mafuta bado Serikali imekuwa ikiruhusu
uingizaji wa mafuta kutoka nje.
Susan Lyimo
Mbunge
wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema), ametangaza nia ya kugombea
Jimbo la Kinondoni, kupitia chama chake hiyo ikiwa ni baada ya
kuwakilisha mkoa huo kupitia viti maalumu akiamini kuwa ni wakati wake
wa kuwa mwakilishi wawananchi wa jimbo hilo linaloongozwa na Iddi Azzan.
Abia Nyabakari
Akichangia
bajeti hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Abia Nyabakari (CCM), alisema
anatarajia kwenda kugomnbea Jimbo la Buyungu ambalo linaongozwa na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Mhandisi
Christopher Chiza.
“Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kumuambia Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Buyungu kuwa
nakuja kugombea ubunge katika jimbo hilo naomba aniunge mkono,” alisema
Nyabakari huku akipigiwa makofi.
Seleman Bungara
Mbunge
wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara (CUF), alisema anagombea tena jimbo
hilo na CCM wasitarajie kupata chochote, kwani wameshindwa kufanya
ambayo waliahidi kwa wananchi akitolea mfano barabara ya kilometa 4.5 ya
lami imeshindikana kwa miaka mitano kujengwa.
Dustan Kitandula
Akichangia
katika bajeti hiyo ya Wizara ya Fedha, Mbunge wa Mkinga, Dustan
Kitandula (CCM), aliwataka wananchi wa jimbo lake kumpa nafasi nyingine
ya miaka mitano ili aweze kutekeleza yale yote ambayo walikubaliana
kuyakamilisha.
Kitandula
alisema wapo watu ambao wanajipitisha jimboni humo ila kinachotakiwa ni
kuwapuuza, kwani hawana jipya ambalo wanaweza kulifanya tofauti na yeye
ambaye wameanza naye.
Herbet Mtangi
Hali
kama hiyo ilijitokeza kwa Mbunge wa Muheza, Herbert Mtangi (CCM),
alisema anatarajia kurejea kuomba ridhaa ya wananchi wa jimbo hilo,
hivyo wakiamua kumrejesha atakuwa tayari kuwatumikia.
Salum Barwany
Mbunge
wa Lindi Mjini, Salum Barwany (CUF), aliweka bayana kuwa atagombea huku
akitoa tahadhari kwa CCM, kuangalia mtu ambaye wanataka kumuweka, kwani
ataumbuka na kuwa aibu ndani ya chama hicho na mgombea huyo.
Wabunge
wengine ambao wametumia bunge kutangaza nia ya kurejea kuomba kura na
majimbo yao katika mabano ni Dk. Athuman Mfutakamba (Igalula, CCM),
Seleman Jafo (Kisarawe, CCM), Dk. Faustine Ndungulile (Kigamboni ,CCM),
Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini, CCM), Haman Yusuph Masauni
(Kikwajuni, CCM), Aliko Kibona (Ileje, CCM), mawaziri ni Waaziri wa
Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (Isamini, CCM), Waziri wa
Maji, Profesa Jumanne Maghembe (Mwanga, CCM).
chanzo:gazeti la jambo leo 19 juni 2015
