HUYU NDIYE MKULIMA ALIYEENDA KUCHUKUA FOMU YA KUGOMBEA URAIS CMM
Mkulima
kutoka Kigoma, Elidephonce Bilohe akiondoka baada ya kushindwa kuchukua
fomu kutokana na kutokamilisha malipo ya ada ya fomu hizo. Hata hivyo,
alikamisha baadaye na atachukua fomu leo Picha na Edwin Mjwahuzi
Makada
watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwamo wa darasa la saba, jana
walijitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba kuteuliwa na chama hicho
wagombee urais.
Waliojitokeza
ni Dk Mwele Malecela, Dk Hamis Kigwangalla na Elidephonce Bilole mwenye
elimu ya darasa la saba ambao walifika Makao Makuu ya CCM kati ya saa
nne asubuhi na saa saba kwa staili tofauti kwa ajili ya kuchukua fomu
hizo.
Hata
hivyo, Bilole (43) aliyetembea kwa miguu huku akiwa amebeba chupa mbili
za maji, mfuko wa plastiki na begi dogo jeusi, hakuweza kuchukua fomu
kutokana na kufika katika ofisi hizo akiwa hana Sh1 milioni za malipo.
Baadaye alifanikiwa kulipa ada hiyo na sasa amepangiwa kuchukua fomu yake leo saa 10.00 jioni.(P.T)
“Nilikuwa
Benki ya CRDB, nikaitwa ofisi za chama nikaona nije ili nisikilize
wito, kabla ya kuchukua fedha kwanza,” alisema Bilole aliyefika peke
yake kwenye ofisi hizo.
Bilole alisema anajua Mungu atamwezesha kukabiliana na watu wengine walioomba ridhaa ya chama kuwania nafasi hiyo.
Alipoulizwa
sababu ya kufika pekee yake katika ofisi hizo, alisema hajawahi kuwa na
makundi ambayo yameonekana kwa makada wengine... “Nadhani naweza ndiyo
maana nimejitokeza kuwania nafasi hii. Nitawavusha kuwapeleka kwenye
nchi ya ahadi,” alisema na kuongeza kuwa alijiunga na chama hicho mwaka
2003 huku akiahidi kuhakikisha anainua uchumi wa nchi kwa kutumia
rasilimali zilizopo.
Bilole ni nani?
Bilole alizaliwa Januari 21, 1971 katika Kijiji cha Mtala wilayani Kasulu mkoani Kigoma na anajishughulisha na kilimo.
Dk Kigwangalla ataja vipaumbele vyake
Baada ya
kuchukua fomu hizo, Dk Kigwangalla alieleza vipaumbele vitatu alivyosema
atavitekeleza. Aliyataja mambo hayo kuwa ni kupunguza wigo wa walio
nacho na wasionacho, kukabiliana kisayansi na mabadiliko ya tabianchi
katika uchumi na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
“Tanzania
ya leo haiwezi kuendelea kwa fikra zilezile, watu walewale... tunalia
na amani, umoja na upendo, lakini bado kuna haja ya kuwa na mabadiliko.
Lazima tufikiri upya, lazima kuwa na mustakabali mpya wa Taifa la
Tanzania,” alisema Dk Kigwangalla.
Nitashughulikia afya, elimu na uchumi - Dk Malecela
Dk
Malecela ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya
Binadamu (NIMR), alisema ameamua kuchukua fomu baada ya kujitathmini.
“Naona
kuna maeneo ambayo ni vizuri yakatiliwa mkazo katika Ilani ya CCM. Eneo
la kwanza ni upatikanaji wa huduma ya afya kwa watu wote, eneo la pili
ni elimu ya ufundi ili vijana wakitoka shule wawe wabunifu na kuongeza
chachu katika teknolojia na eneo la tatu linahusu uchumi,” alisema.
Kuhusu
Muungano alisema: “Utaendelea kuthaminiwa na kulindwa na pale penye
matatizo kwa pamoja tutajitahidi kuyafanyia kazi na hatimaye kuyatatua.”
Dk Mwele
ambaye anakuwa mwanamke wa pili kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM
katika nafasi hiyo baada ya Balozi Amina Salum Ali, alisema
atashughulikia tatizo la rushwa kwa kubana mifumo inayotoa mianya ya
uozo huo.
Dk Mwele ni nani?
Dk Mwele
alizaliwa Dar es Salaam Machi 26, 1963. Alipata elimu ya msingi katika
za shule za Arusha na Oysterbay jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1969
hadi 1975.
Baadaye
alijiunga na elimu ya sekondari katika Shule za Zanaki, Dar es Salaam na
baadaye Weruweru, Kilimanjaro kati ya mwaka 1976 hadi 1979.
Mwaka
1980 hadi 1982 alisoma kidato cha tano na cha sita katika Shule ya
Sekondari ya Kilakala, Morogoro na baadaye akajiunga na Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT), kwa mwaka mmoja.
Alipata
Shahada ya Kwanza ya Zoolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
baadaye Shahada ya Uzamili katika Elimu ya Wadudu kutoka Chuo Kikuu cha
London, Uingereza na Shahada ya Uzamivu ya Vimelea vya Magonjwa (PhD),
katika chuo hichohicho cha London.
Amefanya kazi NIMR kwa miaka 27 na ana mtoto mmoja Naomi (14).
Chanzo:Mwananchi