UKAWA YATAKATA MIPANGO YOTE IKO HAPA>>>
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umesema kila chama ndani ya umoja huo kiko huru kutoa fomu na kuandaa wanachama wake watakaoshindanishwa katika mchakato wa kuwapata wagombea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Tamko
hilo lilitolewa na viongozi wakuu wa Ukawa baada ya kumalizika kwa
kikao cha siku mbili kilichofanyika Shangani, Zanzibar kujadili hali ya
kisiasa na utaratibu wa kuwapata wagombea wa nafasi za udiwani,
uwakilishi, ubunge na urais.
Mwenyekiti
mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema wagombea wa umoja huo
watapatikana kwa kuzingatia sifa na uwezo wa kila mmoja na nia ya kweli
ya kuleta mabadiliko katika nchi.
“Hakuna
chama kinachozuiwa kutoa fomu kutafuta wagombea katika mchakato wa
ndani wa chama kabla ya Ukawa kufanya uteuzi wa mwisho,” alisema Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema.
Kuhusu mvutano
Kauli
ya Mbowe inakuja wakati kukiwa na wasiwasi miongoni mwa wanachama na
wajumbe wa kamati ya ufundi ya Ukawa kutokana na mvutano wa kila chama
kutaka majimbo fulani ambako kila kimoja kinadhani kinakubalika.
Hata hivyo, Mbowe alisema Ukawa inaendelea kuimarika tangu kuasisiwa kwake na hakuna mpasuko kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
“Hakuna
mushkeli, uhusiano wetu Ukawa unaendelea kuimarika na tutahakikisha
tunasimamisha mgombea mwenye sifa na uwezo wa kutuletea ushindi,
hatutagubikwa na masilahi ya vyama, tunataka masilahi ya Ukawa kwanza
vyama baadaye.
“Ni ndoto Ukawa kumeguka kwa sababu tumetambua umoja ni nguvu na wenzetu wanasubiri kuona tunameguka,” alisema Mbowe katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Gharama za uchaguzi
Alipoulizwa
kuhusu gharama za uchaguzi ndani ya Ukawa, Mbowe alisema ni mapema
kueleza hilo lakini hawatarajii kumwaga fedha kama wanavyofanya baadhi
ya wagombea wa chama tawala katika kutafuta nafasi mbalimbali za uongozi
ikiwamo urais wa Muungano... “Ukawa tunajiamini, tuna uwezo wa kushinda dola.”
Awali,
Mwenyekiti wa CUF ambaye pia mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Profesa
Ibrahim Lipumba alisema kikao hicho kimepata mafanikio makubwa na
kusisitiza kuwa wagombea wa Ukawa watatangazwa baada ya kukamilika
mchakato ndani wa vyama.
Alisema
kwa mwelekeo wa kisiasa baada ya kufanya tathmini, Ukawa ina nafasi
kubwa ya kuingia Ikulu ya Muungano na Zanzibar mwaka huu kutokana na CCM
kushindwa kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.
Alisema
lengo kubwa la Ukawa ni kuwa na Tanzania mpya yenye maendeleo na sera
ya maisha bora kwa Watanzania wote na kuwataka wananchi kuwa tayari
kuyapokea mabadiliko ya kiutawala baada ya Uchaguzi Mkuu.
Mwenyekiti
wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema chama chake si msindikizaji katika
Ukawa na nia yake ni kuona mabadiliko ya kiutawala yanatokea.
Aliwataka Watanzania kuwa tayari kufanya uamuzi mgumu.
“Tayari nimeota ndoto Ukawa wanakamata madaraka ya nchi mwaka huu,” alisema Makaidi.
Katiba mpya
Akizungumzia
Kura ya Maoni ya Katiba inayopendekezwa, Mbowe alisema Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC), haiwezi kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja na
kutaka Kura ya Maoni isitishwe kwa sababu muda wa maandalizi ni mdogo
na imeshindwa kuandikisha wapiga kura kutokana na ukosefu wa vifaa.
