JOHN MNYIKA KUWASILISHA MUSWADA BINAFSI BARAZA LA VIJANA
BUNGENI TAREHE 31 MACHI 2015 MUSWADA BINAFSI WA BARAZA LA VIJANA LA TAIFA KUJADILIWA
Nashukuru
wote ambao mmekuwa mkifuatilia hatma ya muswada binafsi wa Baraza la
Vijana la Taifa niliouwasilisha tarehe 31 Oktoba 2013.
Vijana
na wadau wa maendeleo ya vijana mzingatie kwamba muswada huo hatimaye
umepangwa kusomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa Bungeni Jumanne tarehe
31 Machi 2015 katika Mkutano wa 19 wa Bunge.
Muswada
huo ulisomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa 14 wa Bunge tarehe 21
Disemba 2013. Maoni kutoka kwa wadau yalikusanywa Oktoba 2014 na Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii.
Baraza
la Vijana la Taifa pamoja na malengo mengine litawezesha vijana kuanzia
kwenye vijiji/mitaa mpaka taifa kuweza kuwa na vyombo vya kuwaunganisha
vijana kwa kike na wa kiume kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa.
Aidha,
Baraza hilo litafuatilia pia kwa karibu utekelezaji wa mipango ya
maendeleo ya vijana ikiwemo kuhusu ajira, elimu na sekta zingine katika
Halmashauri, Serikali kuu, katika vyombo mbalimbali vya maendeleo na
wadau wa maendeleo.
Pia,
Muswada huo utawezeshwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na
kulipa jukumu Baraza la Vijana kufuatilia kwa karibu utendaji wa Mfuko
wa Maendeleo ya Vijana; kuhakikisha kwamba fedha zinatengwa za kutosha
na kufika kwa walengwa kuwawezesha vijana kujiajiri, kukuza vipaji vyao
na kushughulikia maendeleo yao kwa ujumla.
Kujadiliwa
kwa muswada huo ni hatua ya pekee katika historia ya harakati za vijana
nchini kwa kuzingatia kuwa Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya
mwaka 1996 ilitamka kwamba kutaanzishwa Baraza la Vijana na suala hilo
kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007.
Hata
hivyo Serikali imekuwa ikikwepa kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera
tajwa yanatekelezwa kwa wakati pamoja na kuwa suala hilo linahusu
mustakabali wa maendeleo ya vijana nchini.
Natambua
mchango wa vijana na taasisi zote za vijana mlioshiriki katika
maandalizi ya muswada huu, unaitwa binafsi kwa sababu tu ndio neno
linalopaswa kutumika kwa mujibu wa Kanuni za Bunge lakini ukweli ni
kwamba huu ni muswada wenu; mimi ni mwakilishi.
John Mnyika (Mb)
Machi 2015
