Mbowe aibua mapya mfumo wa BVR, Asema mtaalamu alionya Tanzania haijawa tayari, Usajili ukiendelea utasababisha machafuko ya kisiasa.
Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amedai
kuibua nyaraka zinazoonyesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec),
ilishauriwa na mtaalamu wa mashine za BVR kutoka Marekani kuwa Tanzania
haijawa tayari kwa teknolojia hiyo.
Akifungua
kikao cha baraza la uongozi wa chama hicho Kanda za Nyanda za Juu
Kusini jana alisema, Mshauri Mwelekezi kutoka Marekani Darell Geusz
ambaye ni mtaalam wa mashine za usajili wa wapiga kura kutumia mfumo wa
kieletroniki (BVR) alichukuliwa kuishauri Tume kuhusu mashine hizo.
Alisema
nyaraka hizo zinaonyesha ushauri uliotolewa na mtaalam huyo kwa Tume
ni kuwa Tanzania haijawa tayari kwa teknolojia hiyo kwa sababu hakuna
vifaa, utaalam na wataalam.
“Mtaalamu huyo alishauri wakilazimisha kuendelea kuzitumia mashine hizo watasababisha machafuko ya kisiasa nchini,” alisema.
Mbowe pia alitoa nyaraka nyingine zinazoonyesha jinsi Nec imekuwa ikiandaa kwa siri utaratibu wa BVR bila kuwashirikisha wadau.
Wakati
Mbowe akiibua madai hayo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Tanzania
Bara), John Mnyika, alisema kauli ya Jaji Mstaafu Damian Lubuva dhidi
ya viongozi wa siasa aliyoitoa juzi imelenga kufunika kombe
mwanaharamu apite.
Juzi
Jaji Lubuva aliwaasa viongozi wa siasa kutotumia uboreshaji wa Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura kama mwanya wa kuanzisha fujo.
Mnyika alisema Chadema hakitanyamaza bali kitaendelea kutaka upungufu katika mashine za BVR kufanyiwa kazi.
Alisema
chama chake kimenasa taarifa za mawasiliano kati ya Tume na Taasisi
ijulikanayo kama, IPSITI zikionyesha kwamba Nec haijafanya marekebisho
ya mapungufu yaliyopo kwenye BVR.
Alisema
serikali hususan Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anapaswa kujitokeza
hadharani kuelezea sababu za kutoshughulikia upungufu ulio onekana
licha ya ripoti ya wataalam kubainisha.
Pia
alisema Pinda anapaswa kuueleza umma sababu za serikali kutotoa fedha
kamili kwa Tume hiyo ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa ni pamoja
na kutoa elimu kwa wapiga kura.
“Pinda
awaeleze Watanzania ukweli kuwa Serikali haina fedha kwa sababu
wahisani walisitisha misaada ya kibajeti, hii ilitokana na kashfa za
ufisadi wa kifedha,” alisema na kuongeza:
“Wahisani
walisitisha fedha za misaada ya kibajeti kabla ya bunge halijafikia
maamuzi ya sakata la Akaunti ya Escrow, misaada mingine iliyositishwa
inahusu sekta ya maji na afya, ndiyo maana miradi mingi kwenye
Halmashauri sasa haisongi mbele,” alisema.
Mnyika alisema mkutano ujao wa bunge wataenda kuyaeleza kwa kina kuhusu misaada hiyo ya maji na afya iliyositishwa.
“Leo
tunapata madhara syo tu miradi ya kimaendeleo kukwama, wananchi
wanakosa huduma muhimu za afya na maji kwa sababu ya fedha kutumika
kwenye mianya ya ufisadi badala ya maendeleo,) “ alisema na kuongeza:
“Ukosefu
huu wa fedha umeathiri pia tume katika zoezi muhimu kwa ajili ya
uchaguzi utakaowawezesha Watanzania kupata viongozi bora na kuzuia
mianya ya ufisadi,” alisema.
Alisema
kitendo cha Jaji Lubuva kuvinyamazisha vyama vya siasa wakati BVR zina
upungufu ni sawa na funika kombe mwanaharamu apite.
Mnyika
alisema chama chake kitaendelea kuzungumzia udhaifu na upungufu huo
ambao mwisho unaweza kusababisha watu kuandikishwa zaidi ya mara moja.
Alisema endapo watanyamaza nchi itaingia katika machafuko kwa kuwa upungufu uliopo kwenye mashine hizo ni mkubwa.
“Kuacha
kujadili suala hili nchi itaingia katika hasara ya kutumia fedha
kwenye uandikishaji wakati huo, hii ni kuruhusu mianya ya uchakachuaji
wa uchaguzi na kusababisha kutokuwa huru na haki,” alisema.
Aidha
chama hicho kimeonyesha wasiwasi wa kutokamilika kwa zoezi la
uandikishaji mwezi Aprili 30 kama ilivyotakiwa kutokana na siku ambazo
zitakazotumika kila mkoa.
“Lubuva
amesema Njombe watatumia siku 28 wasiwasi wetu ni kwamba ikiwa siku
hizi zitatumika na maeneo mengine, itafika Aprili 30, baadhi ya maeneo
yatakuwa hayajakamilisha zoezi,” alisema.
Aidha, kutokana na wasiwasi huo, wamemtaka Rais Jakaya Kikwete asogeze mbele hadi uchaguzi mkuu utakapomalizika ndipo lifanyike.
Pia
Mnyika amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda aeleze lini kamati ya
bunge itakutana na Tume ili kuepusha nchi kuingia katika machafuko.
Kuhusu
kauli ya Tume ya kuvitaka vyama vya siasa kusaidia kutoa elimu
uandikishaji kwa wananchi, Mnyika alisema chama chake kimeitikia wito
huo na kina kusudia kwenda mkoani Njombe kuzindua kampeni ya elimu ya
mpiga kura maarufu kama ‘R to R BVR’ ikimaanisha Region to Region BVR.
Hata hivyo, alisema baada ya kupeleka taarifa jeshi la polisi
kuhusiana na mkutano wa uzinduzi huo, wamekataliwa kufanya hivyo kwa
maelezo kuwa kutakuwa na zoezi la uandikishaji huo.
Alisema
licha ya polisi kuzuia lakini wataendelea na zoezi hilo na kumtaka
Mkuu wa jeshi hilo awaagize polisi kupokea mikutano hiyo ambayo
imekusudiwa kufanyika kila mkoa.
CHANZO: NIPASHE
