MADENGE AWATAKA WAISLAMU KUIGA MBINU ZA WAKRISTO KUCHANGIA MAENDELEO YA DINI YAO
| Akipewa zawadi baada ya kuuzindua mpango huo |
| Baadhi ya waumini walioshiriki uzinduzi huo |
MJUMBE
wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mahamudu Madenge
amewasihi waumini wa dini ya kiislamu nchini kote kutumia mbinu za
wakristo kuchangia shughuli zake za maendeleo badala ya kuendelea
kuzilalamikia changamoto zao kwa mamlaka au watu wasiohusika.
Aliyasema
hayo mjini Iringa jana, mbele ya waumini wa dini hiyo walioshiriki
uzinduzi wa mpango mkakati wa mwaka 2015 hadi 2017 wa taasisi ya
kiislamu ya Dhi Nureyn Islamic Foundation yenye makao yake mjini hapa.
Katibu
Mtendaji wa taasisi hiyo, Elm Shamsi aliyataja malengo ya mpango
mkakati huo kuwa ni pamoja na kuondoa utegemezi kwa kujitafutia kipato
kutokana na rasilimali chache walizonazo, kuitangaza taasisi ndani na
nje ya nchi, na kusambaza elimu ya dini.
Mengine
ni kutoa huduma bora za afya katika vituo vyake vya kutolea huduma,
kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule zake, kuboresha huduma kwa
watoto yatima wanaolelewa katika vituo vyao na kuwasaidia vijana
kujipatia ajira kwa kuwapa stadi za maisha kupitia vyuo vya ufundi.
Huku
akiichangia Sh Milioni moja taaasisi hiyo, Madenge alisema maendeleo ya
dini hiyo ni kama yanasuasua kwasababu baadhi ya waumini wake
wanasubiri yaletwe au yachangiwe na watu wengine.
Akitoa
mfano wa jinsi wakristo wanavyoshiriki katika kuiendeleza dini yao,
Madenge alisema katika harambee zao za mara kwa mara za ndani na nje ya
makanisa yao, wapo wanaoweza kununua chupa ya maji ya Sh 500 hata kwa Sh
Milioni moja ili mradi kinachokusanywa kina lengo kufanikisha maendeleo
ya dini hiyo.
“Kwa
mfano hapa Iringa, dini hii ina watu wenye uwezo sana lakini ni mara
chache sana kuwaona wakishiriki au kuchangia shughuli za kuendeleza
uislamu. Katika hili waislamu tunatakiwa kujinyoshea vidole kabla ya
kuwanyoshea wengine,” alisema.
Awali
Kaimu Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Aboubakar Chalamila alionesha
kushangazwa kwake na namna wakristo wanavyoisambaza dini yao kwa kasi
kubwa tofauti kabisa na waislamu.
Akitoa
mfano, Sheikh Chalamila alisema; “lipo dhehebu jipya kabisa la kikristo
mkoani Iringa, dhehebu la Orthodox, nadhani halina zaidi ya miaka kumi
lakini lina makanisa 37 katika maeneo mbalimbali ya mkoa wetu.”
Wakati
kanisa hilo la mfano likikua kwa kasi kubwa, alisema kasi ya waislamu
kusambaza dini yao na kuhakikisha huduma zake zinakuwa jirani na
mazingira yao ni ndogo.
“Mfano
taasisi hii ya Dhi Nureyn inayofanya kazi kwa kutegemea zaidi nguvu za
wahisani toka nje, tangu ianzishwe miaka 29 iliyopita imejenga misikiti
150 katika maeneo mbalimbali nchini. Misikiti hiyo ingekuwa imejengwa
mkoani Iringa pekee tungesema ni mingi lakini kwa kuwa ni nchi nzima ni
michache sana kulingana na mahitaji ya kusambaza uislamu kila mahali,”
alisema.
Awali
Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo, Elm Shamsi alisema utegemezi wa
misaada ya wahisani hasa wa nje ni changamoto inayosababisha taasisi
kukosa chanzo endelevu cha mapato kwa ajili ya maendeleo ya dini hiyo.
Katika kuutekeleza mpango mkakati huo, alisema taasisi inatarajia wadau na jamii inayolengwa watachangia.
Alisema
katika kila idara mkakati umelanga kufanikisha mambo makuu matano
ambayo ni uzalishaji mali, kujitangaza, tathimini na ufuatiliaji,
mafunzo na kuimarisha ushirikiano na wadau wengine.
Mbali na Sh Milioni moja iliyochangwa na mjumbe huyo wa NEC, waumini wengine walioshiriki uzinduzi huo waliichangia taasisi hiyo Sh 348,000.
Mbali na Sh Milioni moja iliyochangwa na mjumbe huyo wa NEC, waumini wengine walioshiriki uzinduzi huo waliichangia taasisi hiyo Sh 348,000.