WALIMU DAR WAANDAMANA KUDAI HAKI ZAO

ZAIDI ya walimu 200 wa shule za msingi na sekondari za Manispaa za Kinondoni, Dar es Salaam jana wameandamana hadi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo wakitaka kutekelezewa madai mbalimbali wanayoidai manispaa hiyo, zikiwamo fedha za likizo pamoja na kupandishwa madaraja.
Walimu
hao wa shule za msingi na sekondari walinza kuandamana saa 5.00 asubuhi
katika Ofisi za Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kinondoni
walipokwenda kuhoji juhudi za chama hicho katika kushughulikia matatizo
yao.
Baada
ya kufika katika ofisi hizo, walimu hao walianza kutoa shutuma kwa
uongozi kwa kutoshughulikia madai yao kikamilifu na hivyo kuwafanya
waendelee kuteseka, hatua iliyowafanya kuwalazimisha viongozi hao
kuongozana nao hadi kwa Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Mussa Natty.
Huku
wakiimba nyimbo mbalimbali za mshikamano ukiwamo wa ‘Solidarity
Forever’ (Mshikamano daima), walimu hao na viongozi wa CWT walikwenda
kwenye ofisi ya Manispaa ya Kinondoni kwa lengo la kuonana na mkurugenzi
lakini walizuiliwa getini.
Hata
hivyo, pamoja na kuzuiliwa na askari wa Manispaa ya Kinondoni kuingia
ndani ya ofisi za manispaa hiyo, walipenya kwa kutumia njia mbalimbali
zinazozunguka ofisi hizo na kuwaacha walinzi wakishindwa la kufanya.
Aidha,
walipoingia ndani ya ofisi hizo, walimu hao waliendelea kuimba nyimbo
mbalimbali huku wakimtaka Mkurugenzi kujitokeza na kuzungumza nao ili
ajue hatma yao huku wakisisitiza kutoondoka eneo hilo kama kiongozi huyo
asingejitokeza.
Hali
hiyo ilifanya baadhi ya wafanyakazi wasitishe kazi kwa muda na
kuchungulia madirishani na wananchi waliokwenda kupata huduma wakapatwa
na mshangao wa kilichokuwa kikiendelea.
Baada
ya dakika 20 tangu walimu hao kuwasili mahali hapo, Mkurugenzi huyo
alijitokeza na kuzungumza nao na kuahidi kulishughulikia suala hilo
haraka iwezekanavyo na kuwataka kusubiri majibu yao ndani ya kipindi cha
mwezi mmoja kuanzia jana.
Baada
ya majibu hayo, walimu hao wakiongozwa na viongozi wa CWT waliondoka
eneo hilo na kuongozana hadi ofisi za chama hicho kwa kikao cha muda
mfupi kilichotoa uamuzi wa walimu hao kuendelea na majukumu yao kusubiri
utekelezaji ulioahidiwa na Mkurugenzi wa Kinondoni wa kushughulikia
madai yao.
Mwalimu
mwingine Huruma Minga, alisema madai ya walimu hao katika manispaa hiyo
ni mengi na mengine yanakatisha tamaa huku akishangazwa na utaratibu wa
upandishwaji wa madaraja unavyofanyika kwa madai kuwa kuna upendeleo.
“Kuna
wakati mtu unajaza fomu ya likizo na pengine kwa utaratibu wako
unatakiwa ulipwe fedha kiasi cha Sh 400,000 lakini unaweza kujikuta
ukilipwa Sh 60,000 na wakati huo hata ile fomu ya likizo ulioijaza
hujajua mahali ilipopelekwa, hivyo kujikuta unapoteza haki yako,” alisema Huruma.
Mbali
na hilo alisema utaratibu wa kuwapandisha madaraja walimu katika
manispaa hiyo una mianya ya upendeleo kwa baadhi ya walimu na kwamba
hadi sasa wapo baadhi hawajapanda hata daraja moja katika kipindi cha
zaidi ya miaka kumi ya ufundishaji.
Alisema
lakini wapo wengine ambao kila baada ya miaka miwili wanapanda madaraja
huku, akidai kushangazwa na walimu waliopo masomoni kutopewa barua za
kupanda madaraja hayo.
Akizungumzia
maandamano hayo, Katibu wa CWT wilaya ya Kinondoni Stephen Mnguto,
alisema hatua hiyo imetokana na walimu hao kuchoshwa na ‘ubabaishaji’ wa
viongozi wa manispaa hiyo jambo ambalo hata wao liliwafanya wasiaminike
mbele ya wanachama wao.
Alisema
kimsingi madai ya walimu hao yangeweza kuwa yamemalizwa kwa kuwa mengi
yana muda mrefu hivyo hakukuwa na haja kulimbikizwa hadi muda huu wakati
suala hilo lipo wazi.
“Yapo
madai ya walimu kutopandishwa madaraja kwa wakati, katika kipindi cha
mwaka 2013/ 14 zaidi ya walimu 1,743 walitakiwa kuwa wamepandishwa
madaraja lakini hadi leo hakuna lililotekelezwa,” alisema Mnguto.
Alisema
licha ya madai hayo yapo madai ya baadhi ya walimu waliopo masomoni
kutopewa barua hizo achilia mbali fedha za likizo alizodai kuwa
hazijatolewa kwa walimu zaidi ya 300.
Hata
hivyo, kupitia katibu huyo, walimu hao walisema wanasubiri utekelezaji
huo huku wakisubiri kujua hatua zipi wazichukue endapo suala hilo
halitotekelezwa kama walivyoambiwa.
Kwa
mujibu wa Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba katika taarifa yake
aliyoitoa bungeni Novemba mwaka jana, walimu nchini walikuwa wakiidai
serikali jumla ya Sh bilioni nne.