URAIS UKAWA 2015 WAKAMILIKA
Dar es Salaam. Wakati CCM ikisubiri Februari kufanya tathmini kuona kama baadhi ya wagombea wake wa urais wametekeleza masharti ya adhabu zao, washindani wao wa Ukawa, Jumanne ijayo watakutana kujadili mambo mbalimbali, ukiwamo mchakato wa kuwapata wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani, imefahamika.
Tangu mwaka huu uanze zimekuwapo
pilikapilika nyingi za kisiasa ndani ya vyama vya siasa na Jumanne
iliyopita CCM ilifanya kikao cha Kamati Kuu mjini Zanzibar na kutoa
maazimio yanayogusia mchakato huo lakini ikasita kutaja ratiba rasmi ya
mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM.
Wakati hali ikiwa
hivyo, habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi ya viongozi wa
Ukawa, umoja huo utakutana jijini Dar es Salaam Januari 20, ukiwa na
ajenda mbalimbali kuhusu ushirikiano wao, likiwamo suala la kupata
wagombea huku vikao vya ndani ya vyama vikitarajiwa mwishoni mwa mwezi
huu.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia alithibitisha
jana kuwapo kwa kikao hicho Jumanne akisema kutakuwa na ajenda nyingine
lakini: “Suala la kupata wagombea nalo huenda likajadiliwa. Kuhusu
suala la mgombea urais wa Ukawa, linaweza kuwa sehemu ya mazungumzo
lakini halipo kwenye ajenda.”
Ajenda nyingine alizotaja ni
mwongozo wa Ukawa, kura ya maoni ya Katiba, changamoto za uandikishaji
wa daftari la wapigakura, hali ya uchumi na tathmini ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa uliomalizika Desemba mwaka jana. Mbatia, ambaye pia
ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alisema watajadili ajenda hizo ili
kuhakikisha wanatafuta majibu ya changamoto zilizopo kwa sasa.
Kiongozi
huyo pia alithibitisha taarifa kuwa kila chama ndani ya Ukawa kupitia
vikao vyake kitateua majina ya wagombea ambao watashindanishwa ndani ya
umoja huo, akisema kabla ya Machi, jina la mgombea urais ndani ya
chama chake litakuwa limeshapendekezwa.
Awali, Katibu Mkuu wa
NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema vikao vya chama hicho
vinavyotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu vitakuwa na ajenda ya
uchaguzi vitakavyojadili mwelekeo wa uchaguzi huo kama kalenda yake
inavyosema.
“Nadhani vikao hivyo ndiyo vitaanza kujadili
ajenda ya uchaguzi ujao. Tulishatoa nafasi ya watu kujitokeza kwenye
nafasi mbalimbali. Tukishapendekeza majina ya wagombea kwa baadaye
ndiyo tutawapeleka ili kuchambuliwa kwa pamoja na kamati ya Ukawa.
“Mpaka
sasa kamati ya Ukawa inaendelea na kazi yake tangu Oktoba mwaka jana
ila inakuwa vigumu kwa wajumbe kujua kazi zote zinazofanywa na kamati
hiyo kutokana na msingi wa majukumu yake.”
Nyambabe alisema
kamati hiyo imekuwa ikifanya kazi, ikijumuisha wajumbe wasiopungua
watatu kutoka kila chama ili kufanya tathimini, kuchambua na kuratibu
shughuli zote za uchaguzi.
Kuhusu
kupata mwongozo wa Ukawa, Nyambabe alisema: “Namna ya kupata mgombea,
ilani moja na mwelekeo, vinaweza kuonekana kuanzia Februari baada ya
vyama kukaa vikao vyake.”
Wakati Nyambabe akisema hayo,
kumekuwa na taarifa katika vyombo vya habari kuwa CUF kimeshatangaza
kumsimamisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwania urais, ambazo hata hivyo,
zimekanushwa na Naibu Katibu Mkuu wake Bara, Magdalena Sakaya.
Alisema
kikao cha hivi karibuni ndani ya chama hicho kilikuwa na ajenda ya
kutathimini Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tu na hakukuwa na ajenda
nyingine iliyojadiliwa. “Bado hatujapendekeza jina lolote,” alisema
Sakaya.
Hata hivyo, Sakaya alisema kikao kijacho cha
wenyeviti wa Ukawa hakitakuwa na mamlaka yoyote ya kuamua au kupitisha
jambo bila kupata baraka za viongozi wa Baraza la Uongozi Taifa kutoka
kila chama.
“Kikao hicho sijafahamu ajenda yake lakini
ifahamike tu kwamba, ndani ya Ukawa kuna vikao vitatu; kikao cha
maofisa, kikao cha makatibu na kikao cha wenyeviti na hufanyika kwa
kuzingatia ratiba zake,” alisema na kuongeza:
“Kwa hivyo
utaratibu wa mgombea hauwezi kupatikana kwa sasa kwani hakuna chama
ambacho kimejadili ajenda yoyote au kupitisha majina ya wagombea wake.”
Sakaya
alisema kabla ya kujadiliwa ndani ya Ukawa, vikao vya mabaraza na
kamati kuu za vyama husika vitakuwa vimeshiriki kuchambua na kupitisha
majina ya wagombea wake wanaokidhi vigezo.
“Baada ya hapo
ndipo majina yatafikishwa Ukawa na kamati itachambua wanaoweza kusimama
kwa niaba ya Ukawa kutokana na tathimini yao watakayokuwa wameipata,”
alisema na kuongeza:
“Kwa upande wa CUF, kalenda yetu
inaonyesha kuwa na vikao mwishoni mwa mwezi huu. Nadhani kutakuwa na
mwelekeo juu ya uchaguzi ujao.” Viongozi wa juu wa Chadema jana
hawakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini Ofisa Habari wake,
Tumaini Makene alisema kwa sasa chama hicho hakijafikiria kuwa na vikao
vyenye ajenda ya kuangalia jina litakalopitishwa kwa ajili ya kuingia
Ukawa...
“Bado kabisa kuhusu suala la kujadili mgombea urais
wa Ukawa, hatujafikiria hilo ila kinachotuumiza akili kwa sasa ni kero
za daftari la wapigakura na kuwapo kwa tume isiyokuwa huru ya uchaguzi.
Ratiba ya ajenda hiyo ikitoka tutajulishana,” alisema Makene.