HALI NI TETE KWA VIGOGO ESCROW.......WENGINE WALIOPATA MGAWO KUPELEKWA MAHAKAMANI LEO, NGELEJA, LISSU WATUNISHIANA MISULI
HALI inazidi kuwa tete kwa vigogo kadhaa wa Serikali juu ya sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, baada ya kuwapo taarifa kuwa wengi watafikishwa mahakamani.
Iwapo
leo vigogo ambao majina yao yamekuwa yakitajwa tangu juzi watafikishwa
mahakamani, wataongeza idadi baada ya juzi watumishi wawili wa Serikali
kufikishwa katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Jana
asubuhi baadhi ya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), walionekana wakiranda katika viwanja vya mahakama hiyo.
Mmoja
wa maofisa hao alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya kuwapo kwao
eneo hilo, alisema wapo kwenye maandalizi ya kuwapandisha kizimbani
vigogo wengine.
Hata
hivyo, ilipotimu saa 7 za mchana, ofisa huyo alisema kuna baadhi ya
nyaraka za watuhumiwa zilikuwa zinarekebishwa kabla ya kufika
mahakamani.
Baadhi
ya watuhumiwa ambao jana walipigiwa simu na kutakiwa kufika Takukuru,
inaelezwa hawakupokea simu kwa hofu ya kuburuzwa mahakamani. Hadi
tunakwenda mitamboni harakati hizo zilikuwa zimekwama.
Watumishi
waliofikishwa mahakamani juzi ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Majunangoma
ambaye alisomewa mashtaka ya kupokea rushwa ya Sh milioni 323.4
zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow kutoka kwa Mkurugenzi wa
Kampuni ya VIP Engeering James Rugemalila.
Kabla
ya Rugonzibwa kufanya kazi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, alikuwa mwanasheria wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (RITA),
ambako alihusika na mufilisi wa Kampuni ya IPTL.
Rugonzibwa,
aliichunguza IPTL, alisimamia watumishi wake wakati kampuni hiyo iko
katika mufilisi na alisimamia mashauri mbalimbali yanayoihusu.
Mshitakiwa
mwingine, ni Theophillo Bwakea ambaye alifikishwa mahakamani kwa kosa
la kupokea rushwa ya Sh milioni 161.7 kutoka kwa Rugemalila.
Bwakea
ni Mhandisi Mkuu wa Mradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), na kabla
ya kufanya kazi huko, alikuwa Wizara ya Nishati na Madini, kitengo cha
kusimamia umeme, ambako anadaiwa alishiriki kutunga sera ya kampuni
binafsi kuuza umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na ilipoanza
kutumika, Kampuni ya kufua umeme ya IPTL ilikuwa ya kwanza kupata
zabuni.
Ngeleja agoma
Katika
hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala, William Ngeleja, amewagomea wajumbe wa kamati hiyo waliomtaka
ajiuzulu kutokana na kutajwa kuhusika na mgawo wa fedha za Escrow.
Pamoja
na hatua hiyo, wajumbe walimtaka Ngeleja ajizulu au akae pembeni ili
kumpisha makamu mwenyekiti aongoze vikao jambo ambalo alilipinga.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mnadhimu wa Kambi ya
Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye ni mjumbe kwenye kamati hiyo,
alisema tangu kuanza kwa vikao hivyo Januari 13, mwaka huu, Ngeleja
amekuwa akiviendesha kwa nguvu licha ya wajumbe kumtaka akae pambeni.
“Amekuwa
akiendesha vikao tangu juzi na hata juzi aliendesha na kuondoka saa 4
na kumwachia makamu wa kamati hii kumshikia,” alisema.
Alisema
juzi baada ya Ngeleja kukaa na kuanza kuendesha kikao hicho, alimtaka
kuachia kiti hicho kama ambavyo maazimio manane ya Bunge yalivyowataka
wenyeviti waliotajwa kuhusika katika kashfa hiyo ya Tegeta Escrow ambapo
yeye anadaiwa kupewa mgawo wa Sh bilioni 40.4 kinyume na sheria.
Lissu
alisema pamoja na kumshauri kuachia ngazi, bado Ngeleja aligoma kwa
madai akifanya hivyo ataonyesha wazi kuwa alihusika katika kashfa hiyo.
“Ngeleja
alisahau katika azimio la Bunge, halikusema wale waliotuhumiwa walikuwa
wezi, lakini akashindwa kujua katika azimio jingine Bunge lilitaka
vyombo vya uchunguzi kuchunguza ili watakaobainika wachukuliwe hatua
ambazo zitathibitisha kama walihusika au la,” alisema Lissu.
Alisema
sheria ya maadili ya uongozi wa umma, inawataka viongozi wa umma
kutojihusisha na migongano ya kimaslahi na vitendo vya rushwa.
“Kwa
mujibu wa sheria za utumishi wa umma, Ngeleja baada ya kutajwa katika
ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
akihusishwa kupokea fedha hizo, ilitosha atangaze kujiuzulu,” alisema
Lissu.
Alisema kama Ngeleja, ataendelea kukiuka uamuzi wa Bunge, suala hilo watalirudisha bungeni ili lijadiliwe upya.
Zitto
Akizungumzia
kuhusu suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alimsihi Ngeleja kutekeleza maamuzi ya
Bunge kwa kuachia nafasi hiyo.
“Namsihi Ngeleja kama kijana mwenzangu atekeleze maamuzi ya Bunge na aache kumtega Spika Anne Makinda,” alisema.
