Wasiofanya Usafi Kupigwa Faini 50,000/-




MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amesema wafanyabiashara watakaokaidi kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi watapigwa faini ya Sh 50,000 papo kwa hapo.

Aliyasema hayo mjini Kibaha mara baada ya kumaliza kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Kibaha wakati wa kutekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli la kila mkoa kufanya usafi kila mwezi.

Alitoa kauli hiyo kufuatia baadhi ya wafanyabiashara kufungua biashara zao na kutofanya usafi licha ya kutangaziwa kuwa wanapaswa kufunga biashara zao kwa saa kadhaa kwa ajili ya kufanya usafi wa maeneo yao.

“Inashangaza kuona baadhi ya watu wanakaidi agizo la viongozi wao kwa kutofanya usafi wa maeneo yao huku wakiendelea kufanya biashara kwenye mazingira machafu,” alisema Ndikilo.

Alisema usafi ni suala la kila mtu na si kwa baadhi ya watu, hivyo kila mkazi na mfanyabiashara wa Pwani anapaswa kutenga muda kwa ajili ya usafi wa mazingira.

Aidha, alisema mbali ya kupigwa faini za papo hapo pia watafikishwa kwenye vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani kwa kukaidi agizo la Rais.

“Mbali ya kufanya usafi wa nje hatua inayofuata ni kufanya usafi wa ndani kama vile kwenye maeneo ya mahoteli, migahawa, nyumba za kulala wageni na sehemu nyingine za kutoa huduma kwa watu,” alisema Ndikilo.



Aliwasisitiza wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali yatokanayo na uchafu hasa yale ya mlipuko kikiwamo kipindupindu ambacho kwa Pwani kimedhibitiwa, kwani kwa sasa hakuna mgonjwa hata mmoja.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.