Wanafunzi wajisaidia katika mashamba ya shule.



Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyabitocho, Tarime mkoani Mara, wanalazimika kujisaidia katika mashamba ya shule kutokana na shule hiyo kuwa na matundu machache ya vyoo.

Baadhi ya wanafunzi hao pia wanalazimika kujisaidia katika choo cha shule kwa kupeana zamu baina ya wale wa jinsia ya kike nay a kiume, hali ambayo inawaweka katika mazingira magumu.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Sylvester Daniel, alisema jana kuwa tatizo la choo shuleni hapo lilianza tangu Aprili, mwaka jana, baada ya kilichokuwapo kubomoka.

Alisema shule hiyo yenye wanafunzi 750, ina choo chenye matundu manne tu, hali ambayo imekuwa ikiwalazimu kupata huduma hiyo muhimu kwa shida, huku wengine wakilzimika kujisitiri katika mashamba ya shule yaliyoko eneo hilo.

Kwa mujibu wa Daniel, kitendo cha wanafunzi kujisaidia ovyo hadi kwenye mashamba ya shule, kimesababisha baadhi yao kuumwa matumbo mara kwa mara, hali inayotishia usalama wa afya zao.

"Kwa kweli wanafunzi wana changamoto kubwa na hasa hii ya ukosefu wa matundu ya kutosha ya choo na kusababisha wajisaidie kwa zamu na tena sehemu moja bila kujali jinsi yao,” alisema.

Alisema kutokana na uchache wa matundu ya vyoo, wanafunzi wake walikuwa wakitumia vyoo vya majirani wanaoishi karibu na shule hiyo, lakini baadaye wakawa wanawafukuza kila wanapokwenda kupata huduma hiyo.

Mwalimu huyo alisema ana uhakika siku chache zijazo tatizo la vyoo litakwisha kwa kuwa choo cha matundu 10 kinakarabatiwa. Alisema ili kukidhi mahitaji ya vyoo, shule yake inahitaji matundu 18.
Alisema choo hicho kikikamilika shule yake itakuwa na jumla ya matundu 14 hivyo kubakia manne ili kukamilisha idadi ya yale yanaotakiwa.

Alifafanua kuwa mwaka huu shule hiyo imepokea watoto 145 wa darasa la kwanza 145, hivyo kuifanya kuwa na jumla ya wanafunzi 750, ambao wanahitaji kupata huduma hiyo muhimu wawapo shuleni.

Ofisa Elimu wa Wilaya ya Tarime, Emmanuel Johnson, alipoulizwa kuhusu tatizo hilo, alithibitisha na kusema aliamuru shule hiyo ifungwe, ndipo wananchi wakaanza kushirikiana na uongozi wa shule kukarabati choo cha zamani.

"Kuna upungufu mkubwa wa vyoo, jamii ya pale haikuwa tayari kuchangia ujenzi, lakini baada ya kuagiza ifungwe ili kunusuru afya za wanafunzi, ndipo sasa wananchi wamejitolea kwa hali na mali kukamilisha choo cha matundu kumi," alisema Johnson.

Alisema kuwa wiki ijayo choo hicho kitakuwa kimekamilika kwa vile kazi inakwenda kwa kasi kwa ushirikiano kati ya mafundi na baadhi ya wazazi ili kuhakikisha shule inaondokana na adha hiyo.
CHANZO: NIPASHE
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.