Walimu walilia nyongeza ya ruzuku shuleni



WALIMU na wanafunzi katika Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga, wameiomba serikali kuongeza ruzuku shuleni ili kukabiliana na matatizo mbalimbali kama vile upungufu wa madawati pamoja na ujenzi wa madarasa.

Akizungumza na gazeti hili, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nyasubi Mjini Kahama, Mpena Musa alisema kwa sasa sera ya elimu bure iliyotolewa na Rais John Magufuli imechangia kwa kiasi kikubwa kwa wazazi kupeleka wanafunzi shule.

Alisema kutokana na mwamko huo wa wazazi, umechangia baadhi ya shule kupata wanafunzi wengi kuliko walivyotarajiwa hali ambayo imefanya kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule husika.

Mwalimu Mkuu huyo alisema kuwa katika shule yake ya Nyusubi jumla ya wanafunzi 560 waliofaulu darasa la saba katika kipindi kilichopita walipangiwa kujiunga na shule hiyo, hali ambayo imefanya kuwa na mbanano mkubwa katika madarasa kwani yapo madarasa matatu tu.

“Tunaiomba serikali angalau iongeze fedha shuleni kama ruzuku kwani kwa sasa huwezi kumchangisha mzazi mchango wowote katika shule kutokana na sera ya Rais wetu ya elimu bure kutoka chekechea hadi sekondari na katika shule yangu kuna upungufu wa madarasa 11 huku Halmashauri ya Mji ikiahidi kujenga madarasa mawili kati ya hayo, ”alisema.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakato kata ya Nyasubi wilayani hapa, Mayunga Alphonce amewataka baadhi ya wafanyabiashara mjini hapa kujitokeza kusaidia miche ya miti kwa kuotesha katika shule ya sekondari ya Nyasubi ili kuwasaidia wanafunzi kupata kivuli wakati wa mapumziko.

Mayunga aliyasema hayo wakati wa upandaji wa miti 300 katika sekondari hiyo lililofanywa na wanafunzi wa kidato cha kwanza ambayo ilitolewa na baadhi ya wafanyabiashara wa miti waliopo pembezoni mwa barabara kuu katika Kata Nyasubi eneo la Mtaa wa Nyakato mjini Kahama.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.