TFDA yateketeza bidhaa za mamilioni Singida

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA), Kanda ya Kati imeteketeza bidhaa mbalimbali zilizokamatwa mjini Singida za thamani ya zaidi ya Sh milioni 13.8.

Mkaguzi wa TFDA Kanda ya Kati, Aberl Deule, alisema bidhaa zilizokamatwa na kuteketezwa ni pamoja na vipodozi vilivyopigwa marufuku, vyakula, dawa na vinywaji ambavyo muda wake wa kutumika umekwisha vyote vikiwa na uzito wa tani 3.5.

Alisema bidhaa hizo zilikamatwa kwenye maduka mbalimbali mjini Singida wakati wa ukaguzi wa kawaida uliofanyika kwa muda wa siku 10.

Alisema ukaguzi huo ulifanywa kwa pamoja na maofisa kutoka manispaa ya Singida, lengo kuu likiwa ni kuhakikisha soko la bidhaa siku zote linakuwa na bidhaa bora ambazo hazina madhara kwa binadamu. Aidha, alitoa mwito kwa wafanyabiashara kujenga utamaduni wa kujali afya za wateja wao badala ya kutanguliza mbele maslahi yao binafsi.

Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Singida, Dk John Mwombeki alisema pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maduka pia hutoa elimu kwa wafanyabiashara wote kuhusu umuhimu wa kuwauzia wateja wao bidhaa isiyo hatarisha afya zao.

Wakati huo huo, Dk Mwombeki amewataka watumiaji wa bia kuhakikisha wanakagua vinywaji hivyo kabla ya kuanza kunywa ili kubaini iwapo muda wake wa kutumika bado haujaisha.

Alisema kuwa katika ukaguzi wao wa mara kwa mara wamegundua bia nyingi zinakuwa zimeisha muda wake wa kutumika. Alisema matumizi ya vinywaji vilivyomaliza muda wake ni hatari kwa afya ya mtumiaji hivyo aliwasisitiza watumiaji wa bidhaa nchini, kuhakikisha wanaangalia muda wa matumizi.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.