Sababu za Magufuli kutohudhuria sherehe ya mabalozi


HATUA ya kutoonekana kwa Rais Dk. John Magufuli katika sherehe ya kutakiana heri ya mwaka mpya na wanadiplomasia (Sherry Party), imezua mjadala mzito miongoni mwa Watanzania.

Kutokana na kutokuwapo kwa rais katika sherehe hiyo iliyofanyika juzi Ikulu jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, alimwakilisha na alisoma hotuba kwa niaba yake.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, alisema ilikuwa ni sahihi kwa Rais Magufuli kuwakilishwa na Waziri Mahiga katika sherehe hiyo.

Alisema hatua hiyo ilitokana na Rais Magufuli kuwa nje ya Dar es Salaam, ambapo asipokuwapo huwakilishwa na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu au Waziri wa Mambo ya Nje.

“Rais alikuwa nje ya Dar es Salaam ndiyo maana akawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na ‘Sherry Party’ ni hafla ya kutakiana heri ya mwaka mpya na wanadiplomasia.

“Na Cocktail (mchapalo) hufanyika kila mwaka na huwa ya muda mfupi ambao wanadiplomasia husikiliza hotuba ya rais kuhusu sera yake ya mambo ya nje. Hivyo kwa kuwa Rais Magufuli hakuwepo, hotuba yake ilisomwa na Waziri Mahiga jambo ambalo ni sahihi na hakuna kosa lolote,” alisema Msigwa.

Akizungumza suala la mabalozi hao kuwekewa makatarasi chini, alisema si karatasi za kawaida, huwa zimeandikwa jina la balozi au nchi anayowakilisha ambapo hutakiwa kusimama katika eneo lake husika alilopangiwa.

“Suala la kuwekewa karatasi mbele si geni, huwa linafanyika kila mwaka na pindi zinapowekwa huandikwa jina na cheo cha mwanadiplomasia anayewakilisha nchi husika, na baada ya kusomwa hotuba hupita mbele na kumpa mkono kiongozi.

“Na kwa jana (juzi), aliyesimama mbele alikuwa ni Mheshimiwa Waziri Dk. Mahiga, naibu waziri pamoja na mkuu wa itifaki, na walifanya hivyo kwa sababu walikuwa wakimwakilisha Rais Magufuli katika hafla,” alisema.

Theme images by hanoded. Powered by Blogger.