Ni Kubana Matumizi au Udikteta?


Rais Dk. John Magufuli.

Katika siku zake 100 za mwanzo, Rais Dk. John Magufuli amechukua uamuzi juu ya mambo kadhaa, ambayo baadhi ya wananchi wanayatafsiri kuwa ni viashiria vya udkteta huku wengine wakisema ni kubana matumizi.

Ingawa hivi karibuni akikiwa kwenye kilele cha Siku ya Sheria nchini, alisema yeye si kichaa, mnyama wala dikteta bali anachokifanya ni kuhakikisha mambo yanafanikiwa kwa kusimamia utendaji wa serikali ambao umeharibika.
Kufungiwa kwa chombo cha habari

Januari 15, mwaka huu, serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ilitangaza kulifutia usajili gazeti la Mawio kwa kile kilichoelezwa na Waziri wa Wizara hiyo, Nape Nnauye, kuwa liliandika habari yenye viashiria vya kuvunja amani nchini. 

Kufutwa kwa gazeti hilo, kutochapisha nakala yoyote ngumu au mtandaoni bila kupewa adhabu ndogo iwe ya kuonywa au kujirekebisha, ni dhahiri kulikuwapo na viashiria vya udiktekta ndani ya siku 100.

Bunge kutooneshwa ‘Live’
Januari 26, wakati vikao vya Bunge vikiendelea mjini Dodoma, Waziri Nape alitangaza kusitishwa kwa matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja na Televisheni ya Taifa (TBC) na badala yake yatakuwa yanarekodiwa na kutafutiwa muda wa ziada.

Kauli hiyo ya Waziri Nape inatafsiriwa kama ya udikteta dhidi ya wananchi kwa kuwanyima uhuru wa kupata habari kinachojadiliwa bungeni moja kwa moja.

Amri ya Waziri Nape bila kushauriana na wabunge wengine ambao ndio wawakilishi wa wananchi, inatafsiriwa kuwa udikteta.

Bunge kuingiliwa
Baada ya kulihutubia na kulizindua Bunge la 11, Rais Magufuli alihudhuria hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya wabunge katika viwanja vya bunge mjini Dodoma na kuagiza fedha zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla hiyo, Sh. milioni 225, zipelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kwa ajili ya kununulia vitanda vya wagonjwa.

Bunge ni mhimili wa serikali unaojitegemea katika kutoa uamuzi wake, hivyo hatua ya Rais Magufuli kuingilia kati mambo yake, inatafsiriwa kuwa udikteta, japokuwa uamuzi wake ulikuwa sahihi kwa maendeleo ya taifa.

Kadhalika, hatua ya Rais Magufuli kumteua Dk.Tulia Ackson kuwa mbunge wa kwanza ikiwa ni siku mbili kupita baada ya kuteuliwa na Kamati Kuu ya CCM kuingia kwenye ‘tatu bora’ ya kuwania Uspika, inadhihirisha Rais Magufuli alitumia mamlaka yake kumweka kuwa Naibu Spika wa bunge hilo.

Fedha za Uhuru kutumika katika barabara
Hatua ya Rais Magufuli Desemba Mosi, mwaka jana, kuagiza Sh. bilioni nne zilizokuwa zitumike katika sherehe za maadhimisho ya siku ya Uhuru zipelekwe katika upanuzi wa barabara ya Mwenge- Morocco jijini Dar ea Salaam, yenye urefu wa kilometa 4.3, pia inaweza kutafsiriwa kuwa udikteta.

Kila mwaka ifikapo Desemba 9, Watanzania wamekuwa na destruri ya kusheherekea sikukuu ya Uhuru kwa kujumika katika Uwanja wa Uhuru na kuona maonyesho mbalimbali, likiwamo gwaride linaloandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama.

Lakini Rais Magufuli, baada ya kuingia madarakani, alisitisha kufanyika kwa sherehe hizo, na kuagiza Watanzania waitumie katika kufanya usafi maeneo ya nyumba zao na ofisini.

CHANZO: NIPASHE
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.