Mr Tanzania jela miaka 17, Mwakalebela apanda kortini




RAIA wa Pakistan, Mohammad Nauman Khalilur (32), ambaye pia aliwahi kuwa mshindi wa shindano la Mr Tanzania amehukumiwa kifungo cha miaka 17 jela au kulipa faini ya Sh milioni nne baada ya kukubali mashitaka aliyosomewa, ikiwemo kuishi nchini bila ya kibali.

Mbali na Khalilur, pia aliyewahi kuwa nahodha wa timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’, David Mwakalebela (56) naye amepandishwa kizimbani akikabiliwa na mashitaka ya kutaka kumsaidia mshitakiwa huyo kusema uongo ili kupata hati ya kusafiria ya Tanzania.

Washitakiwa hao walifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Huruma Shahidi na kusomewa mashitaka hayo na Mwendesha Mashitaka kutoka Idara ya Uhamiaji, Method Kagoma.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Shahidi alisema kuwa katika mashitaka ya kwanza mshitakiwa atatakiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh laki tano. Pia alisema kuwa katika mashitaka manne, Mr Tanzania atatakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa au kulipa faini ya Sh 700,000.

Awali, akiwasomea mashitaka hayo, Kagoma alidai kuwa mshitakiwa wa kwanza ambaye ni Mr Tanzania na mtunisha misuli, anakabiliwa na mashitaka sita ikiwemo kuishi nchini bila ya kibali.

Alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari 29 mwaka huu, Makao Makuu ya Uhamiaji Dar es Salaam, akiwa raia wa Pakistan alikutwa akiishi nchini bila ya kibali.

Pia alidai Oktoba 20 mwaka jana, maeneo hayo, akiwa raia wa Pakistan alitoa taarifa za uongo katika fomu za idara hiyo yenye namba 946316 kwa lengo la kupata hati ya kusafiria ya Tanzania.

Katika mashitaka ya tatu, ilidaiwa kuwa alitoa cheti cha kuzaliwa chenye namba 00253800 kwa lengo la kupata hati hiyo, huku akijua kuwa nyaraka hizo ni za kughushi.

Kagoma alidai mshitakiwa pia alitoa nakala ya uraia wa Tanzania ya Amina Mohamed ambayo alimtambulisha kuwa ni mama yake, kwa lengo la kupata hati hiyo.

Pia alidaiwa alitoa hati ya kusafiria ya Amina Mohamed yenye namba AB 228350 kwamba ni mama yake.

Katika mashitaka ya sita, ilidaiwa kuwa Januari 29 mwaka huu, maeneo hayo, alikutwa na taarifa ya uongo ambayo aliweka alama za vidole katika fomu za Uhamiaji, ambayo ilitakiwa kutumiwa na raia wa Tanzania (CTSCAI) yenye namba 09711752.

Kwa upande wa Mwakalebela alidaiwa kuwa Oktoba 20 mwaka jana, akiwa raia wa Tanzania, alimsaidia mshitakiwa kutoa taarifa za uongo huku akijua kuwa sio raia wa Tanzania.

Hata hivyo, Mwakalebela alikana mashitaka yanayomkabili, ambapo kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 17 mwaka huu.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.