MAJIPU YATUMBULIWA TENA: MAJALIWA AWAFUKUZA KAZI WATUMISHI WA VIPIMO NCHINI
WaziriMkuu, Kassim Majaliwa (pichani), amewasimamisha kazi watendaji wawili wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA) ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini kutokana na zuio la kufunga mita kwa zaidi ya miaka mitano.
Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji Mkuu wa WMA, Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha mafuta Bandari, Bernadina Mwijarubi.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Majaliwa, kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Majaliwa alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili.
“Katibu Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi na katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi uchunguzi utakapokamilika na vile vile utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi ziendelee,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu alisema ofisi yake itawaandikia barua Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na polisi ili wafuatilie suala hilo mara moja.
Majaliwa alisema ikithibitishwa kuwa walihusika katika sakata hilo, hatua kali zitachukuliwa na endapo hawakuhusika watarudishwa kazini.
Pia Waziri Mkuu aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow meters uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria usitumike tena.
Juzi Waziri Mkuu alifanya ziara kukagua mita za upimaji wa mafuta bandarini (flow meters) za zamani zilizopo Kurasini na kisha akatembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni.
Katika ziara hiyo alibaini mapungufu mbalimbali na kumtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa vipimo (WMA) Chuwa kuandika barua ya kujieleza ni kwa nini aliamua kufunga mita za upimaji mafuta bandarini.
Majaliwa alizikuta mita hizo zikiwa zimejaa kutu kutokana na kutelekezwa kwa miaka zaidi ya mitano bila kufanyakazi.
CHANZO: NIPASHE