KISIMA CHA MTENDAJI KATA CHA UA WATOTO WAWILI

WATOTO wawili wamekufa baada ya kutumbukia kwenye kisima cha maji kilichopo jirani na makazi yao. Tukio hilo lilitokea Februari 9, mwaka huu saa 10:00 jioni katika kijiji cha Mtakuja kwenye kata ya Nangando wilayani Liwale mkoani hapa, ambapo watoto hao walizama na kufa maji walipokuwa wakicheza na wenzao kando ya kisima hicho.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Polisi wilayani hapa, Raphael Mwandu alisema, watoto hao walifikwa na umauti walipokuwa wakicheza na wenzao jirani na kisima hicho kinachomilikiwa na Mohamed Nguwate (44), ambaye ni Mtendaji wa Kijiji cha Mtawatawa kwenye Kata ya Kiangara wilayani Liwale.

Aliwataja watoto hao kuwa ni Pili Nkoroma (3) mwanafunzi wa shule ya awali Montessori na Asnat Sudi Mtutuma (2) wote wakazi wa kijiji cha Mtakuja. Shuhuda wa tukio hilo, Asha Makumba alisema siku hiyo alikuwa akielekea nyumbani kwa mama yake ndipo alipofika katika eneo la tukio na kuwakuta watoto wakilia na kupiga mayowe huku wakitaja majina ya marehemu hao, na kueleza kuwa wamezama kisimani.

“Nilistushwa na kuogopa, lakini ghafla nilipata ujasiri na kuamua kuwaopoa watoto hao waliokuwa wakielea juu ya kisima,” alisema. Aliongeza kuwa, baada ya kuwatoa watoto hao ambao walionekana kulegea na matumbo yao kuwa makubwa kuliko kawaida, aliamua kupiga yowe zaidi ili apate msaada na ndipo majirani pamoja na wazazi wa watoto hao walipokuja kwenye eneo la tukio na kujaribu kuwapatia huduma ya kwanza bila mafanikio.

Mwanahamisi Ng’oloko ambaye ni mama wa marehemu Pili alisema, baada ya kuona mwanawe yupo katika hali hiyo alimpigia simu mumewe aliyefika na kuwapeleka hospitali ambako, hata hivyo alielezwa na daktari kuwa walikuwa wamekwishapoteza maisha.

Theme images by hanoded. Powered by Blogger.