Kama Unataka Mtoto Wako Awe Na Mafanikio Makubwa, Mpe Malezi Haya.

Kwa mtu anayefikiri kwa makini na anayependa kuyatazama mambo kwa uhalisia, anaweza kukubali jambo hili.  Anaweza kukubali kwamba, kundi la watu wanaofujwa na kuumizwa na mfumo usio wa haki miongoni mwa binadamu, ni watoto.
Mara nyingi tunazungumzia sana kuzalilishwa na kukandamizwa kwa wanawake, lakini ukweli ni kwamba, watoto ndiyo wanaobeba mzigo mzito zaidi katika hilo. Kupunguzwa kazi kwa wazazi, kukosa mahitaji ya msingi kwa familia, na mengine, mzigo wake kwa sehemu kubwa hubebwa na watoto.
Kuna sababu nyingi ni kwa nini watoto ndiyo ambao hubeba mizigo ya familia. Kwanza, ni ile hali ya kuamini kwamba, watoto ni watu wanaostahili kuonywa tu lakini siyo kusikilizwa sana.
Inatokana pia na imani ya wazazi wengi kwamba, watoto ni sawa na ‘mwanasesere’, ambao tumewafinyanga na tunaendelea kuwafinyanga. Hivyo, ni viumbe wasio na hisia, wala makusudi ya kuwa hapa duniani, kama wao.

MWONYESHE MTOTO WAKO KUWA ANAWEZA.
Wazazi wengi huamini sana kwamba, kwa watoto ni lazima kuwe na njia moja ya kufanya mambo, yaani kufanya kwa usahihi. Lakini, usahihi huo ukiwa ni ule utashi wa mzazi, yaani mtoto afanye kama mzazi anavyotaka.
Mtaalamu mmoja wa masuala ya watoto, Dk. T. Berry Brazelton, aliwahi kusema kwamba, mtoto, tangu akiwa mchanga, licha ya kuona na kusikia, lakini pia huwa ana uwezo wa kutambua kile wa kinachotokea kutokana na wazazi wanavyosema au kufanya.
Kwa hali hiyo ni kwamba, watoto ni sawa na watu wazima kihisia. Tunapowatendea kwa njia ambayo tunadhani haitawaumiza kwa sababu ni watoto, huwa tunawakosea sana. Kwa bahati mbaya, huwa tunawaumiza kwa kauli na vitendo vyetu, mara nyingi kuliko tunavyofikiria.
Kwa sehemu kubwa wazazi huwa hawawashirikishi watoto kwenye shughuli za kifamilia au maamuzi, ambayo nao wangeweza kuwa na mchango hata kama ni kidogo. Kuna wakati watoto wana majibu ya matatizo ya familia, lakini hawayasemi kwa sababu hawajapewa nafasi. Kwa kupewa nafasi, wanaweza kujiamini na kusaidia katika utatuzi wa matatizo mbalimbali ya kifamilia.
Jaribu kujiuliza ni mara ngapi tunawashirikisha watoto wetu katika yale tunayoyafanya, ili kusikia nao wanasemaje? Ni kwa kiasi gani tumeweza kuwashirikisha watoto wetu kutoa suluhu kwa matatizo ya kifamilia? Wengi bila shaka tumekuwa tukiwadharau na kuona mawazo yao bado ni madogo sana.
Lakini kitu ambacho wengi wasichojua watoto wanaposhirikishwa kutoa maoni yao, hupewa msukumo wa kujiamini sana, msukumo wa kujitolea kwa wengine na kuhisi hali ya kuaminiwa. Na kwa kujiamini huko hujikuta wakifanya mambo mengi kwa ujasiri bila ya kuogopa kitu. Unajua ni kwanini? Ni kwa sababu wanajua kwamba wanaaminiwa, hivyo, imani ya naweza inakuwa kubwa sana ndani mwao.
Watoto wetu wanapopewa nafasi ya kukua kama wao, hujibaini kwa nafasi kubwa zaidi na kupewa nafsi yenye kuonesha kujali hisia zao na ukamilifu wao kama watu, tunapunguza sana idadi ya mimba za utotoni, vurugu za ujana, maambukizi ya maradhi ya zinaa na mengine ya aina hiyo.
Ni vyema ukatambua kuwa, kama unataka mtoto wako awe ana mafanikio makubwa siku zote mpe malezi haya. Hakikisha unamfanya anajiamini zaidi toka akiwa mdogo. Hilo litafanikiwa ikiwa utachukua hatua ya kumshirikisha baadhi ya mambo, kumpa mawazo chanya na kuepuka kutokumkatisha tamaa kwa namna yoyote ile.
Tunakutakia kila la kheri katika malezi bora ya mtoto wako na endelea kutembelea AMKAMTANZANIA kwa ajili ya kujifunza.
Kwa makala nyingine nzuri za maisha na mafanikio, kumbuka kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kila wakati.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Simu0713 048 035,
E-maildirayamafanikio@gmail.com
Blog;dirayamafanikio.blogspot.com 
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.