Elimu bure shule yajikuta na wanafunzi 5823
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadik amesema kwamba sera ya elimu bure imewezesha wazazi kote nchini kuweza kuandikisha watoto shule jambo ambalo limepandisha idadi ya uandikishaji wa darasa la kwanza mara dufu.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na wazee wa jiji la Dar es salaam kwa ajili ya kumpongeza Rais Dkt. Magufuli kwa kukaa madarakani kwa siku 100 huku akitekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Ameongeza kuwa katika shule ya msingi Maji matitu jijini Dar es salaam imeweza kuandikisha wanafunzi 1,022 wa darasa la kwanza na kuvunja rekodi ya shule zote hapa nchini, Pia shule hiyo moja ina wanafunzi 5823 jambo ambalo kwa mujibu wa viwango vya elimu kwa idadi hiyo ya wanafunzi hao wanatosha kuanzisha shule 6.
Kwa kutambua upungufu uliopo katika shule hiyo kuanzia siku ya jumatatu serikali kupitia mkoa wa Dar es salaam itajenga madarasa 10 katika shule ya Majimatitu wilayani Temeke.Pia Mkoa utajenga madarasa 500 katika manispaa za Ilala,Kinondoni na Temeke ili kuhimili kishindo cha wanafunzi walioandikishwa.
Aisha Mkuu wa mkoa amewataka watanzania wote kumuunga mkono Rais Magufuli katika utumishi wake na kuepuka kumkatisha tamaa kwani nchi inayojengwa ni moja hakuna haja ya kugombea fito.