BAZIL MRAMBA, DANIEL YONA WAACHIWA HURU WATUMIKIE KIFUNGO NJE YA MAGEREZA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeridhia waliokuwa Mawaziri wastaafu Basil Mramba na Daniel Yona kutumikia adhabu ya kifungo cha nje kwa kufanya usafi katika maeneo ya kijamii ikiwemo Hospitali ya Sinza Palestina.
Hatua hiyo inatokana na Mramba ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Yona aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, kupitia Mawakili wao kuwasilisha barua mahakamani hapo kutoka Magereza kuhusu kutumikia kifungo cha nje.
Mawaziri hao wa zamani waliwasilisha barua hiyo ya kuitaarifu mahakama yenye kumbukumbu namba 151/DA/3/11/223 ya Desemba 5, mwaka jana, wakiongozwa na jopo la mawakili wao watatu Peter Swai, Cuthbert Nyange na Elisa Msuya.
Katika barua hiyo waliyoiwasilisha kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘Wafungwa wenye sifa ya kutumikia vifungo vyao chini ya Mpango wa Huduma kwa Jamii”.
Hakimu Mkeha alisema mchakato huo ulianza baada ya Magereza kuwasilisha barua hiyo mahakamani hapo kwa kupeleka majina ya watu wanaotumikia kifungo cha nje ikiwemo mawaziri hao.