Wabunge CCM wamgeuka Magufuli, Wahoji Hatima ya Chama

Rais Dk. John Magufuli*Wahoji bomoabomoa Dar, hatima ya chama
*Lukuvi, Simbachawene wawekwa kitimoto
NA ELIAS MSUYA, DODOMA
WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamemgeuka Rais Dk. John Magufuli na kutaka kasi yake iangaliwe upya vinginevyo inaweza kukigharimu chama hicho tawala kwa wananchi.
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani kumekuwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa ikiwamo kuifumua Bandari ya Dar es Salaam na kusimamisha vigogo kadhaa pamoja na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahaco) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hatua nyingine ni kubomoa nyumba katika bonde la Msimbazi na Mkwajuni jijini Dar es Salaam na kuwafukuza wafanyakazi wageni wasio na vibali.
Wakizungumza katika vikao vya siri vilivyoanza mjini hapa tangu juzi na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, baadhi ya wabunge wanaelezwa kuonyesha hofu ya hatua hizo kuwa huenda zitakigharimu chama chao kwa wananchi.
Wabunge hao wapo mjini Dodoma kwa ajili ya semina ya siku mbili yenye lengo la kupata mbinu za kupambana na kambi ya upinzani ambayo imefanikiwa kuongeza idadi ya wabunge katika Bunge la 11 litakaloanza rasmi wiki ijayo.
Taarifa kutoka chanzo cha uhakika ndani ya vikao hivyo, zilisema kuwa wabunge hao walilalamikia suala la bomoabomoa kwamba linakichafua chama chao mbele ya wananchi na kuhoji kama hakukuwa na njia nyingine za kuwahamisha wananchi hao.
“Wabunge wametaka ubomoaji usitishwe kwa waliojenga ndani ya mita 60, ila afadhali ufanywe kwa walio mabondeni kabisa. Wengine walishauri kuwa ubomoaji ungeachwa kabisa hadi mvua zianze ndipo wawaondoe,” kilisema chanzo chetu.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.