Raisi Magufuli Ampa Siri Nzito Samatta, Wengi Wamtabilia Mafanikio Zaidi

RAIS wa Tanzania Dk John Magufuli amempongeza Nahodha wa timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania (Taifa Stars) Mbwana Samatta kwa kusajiliwa na timu ya KRC Genk inayocheza Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa jana, ilisema katika salamu hizo za Rais Magufuli kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amesema Samatta ameijengea heshima Tanzania na kuitangaza kimataifa.
Rais Magufuli alisema mafanikio ya Samatta kwenda kucheza ligi kubwa duniani, kunafungua milango ya wanasoka wengine wa Tanzania kujiunga na timu kubwa duniani, ambako licha ya kujipatia ajira zenye kipato kizuri, kunaiwezesha kuinua soka lake.
“Nimefurahishwa na mafanikio anayoendelea kuyapata Mbwana Samatta, nawaomba wanasoka wote Tanzania wayachukue mafanikio haya kama changamoto ya kufanya vizuri na kuzivutia timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi,” alisisitiza Rais Magufuli.
Pia Rais alimtaka Samatta kuongeza juhudi akiwa katika timu yake hiyo mpya ya KRC Genk, na amemuombea mafaniko mema yeye mwenyewe na timu yake. Wakati huohuo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi amempongeza Samatta kwa kusajiliwa na timu hiyo ya Ubelgiji.
Malinzi amempongeza Samatta kwa kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya Ubelgiji baada ya kusaini mkataba wa miaka minne kuichezea RC Genk inayoshika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini humo.