Mvua yaacha kaya 30 bila makazi
Aidha mvua zimeharibu ekari 47 za mashamba ya mazao mbalimbali. Diwani wa Kata ya Gulwe, Gabriel Kizige alisema pamoja na maafa hayo pia maji yameingia katika nyumba 50 na kusababisha mali kuharibika ikiwemo chakula.
Akitoa taarifa ya madhara yaliyopatikana mbele ya Kamati ya Maafa, Mwenyekiti wa Kijiji cha Gulwe, Peter Sogodi alisema kuwa nyumba 30 za wakazi wa hapo zilibomoka, nyumba 50 ziliingia maji na ekari 47 za mazao mbalimbali ziliharibika kwa kusombwa na maji.
Aidha Ofisa Mkaguzi wa njia ya treni Stesheni Gulwe, Moses Magoha alisema pia mvua hiyo imesababisha njia ya reli hiyo kufukiwa kwa mchanga na zaidi mita 26 za reli imebomolewa na mvua hiyo.
Akizungumza mmoja wa wananchi, Elizabeth Stephen alisema mvua hiyo ilinza kunyesha majira ya saa 9:00 usiku na kusababisha maafa hayo katika kijiji chao.
Hata hivyo imeelezwa kuwa baadhi ya kaya zilizokumbwa na mafuriko ni zile ambazo awali zilihamishwa kupelekwa maeneo salama na kurejea katika makazi yao ya zamani ambayo ni mkondo wa maji.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mohamed Utaly amewataka waathirika wa mafuriko hayo kutokurudi tena katika makazi hayo ya zamani ambayo ni hatarishi kwa maisha yao.
Aidha alisema katika hatua za awali wananchi hao wataweza kusaidiana na serikali itakayotoa sehemu ya chakula cha njaa kuweza kusaidia kaya zilizoathirika na mafuriko kwa sehemu kubwa.