Mgombea Chadema ashinda udiwani akiwa gerezani
Sumbawanga.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulikuwa na vionjo vyake, ulivutia wengi na
ulikuwa hautabiriki. Haikuwa rahisi kujua nani atakuwa mshindi katika
kiti cha urais hata katika majimbo ya ubunge na udiwani.
Kauli
mbinu ya ‘Mabadiliko’ ilitumika kuwateka wapigakura, aliyekuwa mgombea
wa Chadema katika urais, Edward Lowassa na vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) ndiyo viliitumia kusisitiza muda wa kufanya
mabadiliko umewadia. Upande mwingine mgombea wa CCM ambaye sasa ndiye
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli
akaiiteka na kutafsiri ya M4C ya Chadema kwamba ni ‘Magufuli for
Change’.
Vumbi la
kampeni halikuwa la kawaida kati ya wagombea hao wawili waliokuwa
wakichuana vikali kwa kuwa walikuwa na mvuto wa aina yake na sera za
kipekee.
Yote tisa,
kumi uchaguzi huo ulikuwa na vioja vyake kwa wakazi wa Kata ya Lusaka
iliyopo Tarafa ya Laela wilayani Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa wakaandika
historia ya kipekee kwa kumchagua mgombea aliyekuwa akitumikia kifungo
gerezani ili awe diwani wao.
Aliyechaguliwa
akiwa gerezani ni Ameri Nkulu (56), mkazi wa Kijiji cha Kizumbi,
aliyekuwa mgombea wa udiwani kupitia tiketi ya Chadema, akiibwaga CCM na
vyama vyingine.
Alivyohukumiwa
Oktoba
23, mwaka 2015, Nkulu alihukumiwa kwenda jela kwa miezi sita, ikiwa ni
siku mbili kabla ya wananchi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu
uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Nkulu
alipatikana hatia katika shitaka la kupigana na kiongozi wa CCM kwenye
kata hiyo, Christian Kafwimbi baada ya kufunguliwa kesi namba 33/2015.
Hakimu
Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga, Rozari Mugissa
ndiye aliyemuhukumu Nkulu na mwenzake kwa kutumia kifungu cha adhabu cha
87, sura ya 16 ya Makosa ya Jinai, baada ya kuwakuta na hatia ya kupiga
na kupigana hadharani.
Hata
hivyo, hukumu hiyo iliyomtupa gerezani Nkulu, haikuzuia wakazi wa kata
yake kumchagua kuwa diwani wa Lusaka bali walimpa ushindi kwa kura zao
wakiamini akimaliza kutumikia kifungo atatoka na kuendelea kupigania
maendeleo endelevu ya kata yao.
Mwanasheria
kutoka Kampuni ya S. Mawalla Law Consultants, Mathias Budodi anaeleza
kwamba kwa kosa la aina hiyo, sheria imetoa mbadala katika hukumu kwa
mshitakiwa kutakiwa kulipa faini ya Sh 500 au kifungo cha chini ya mwaka
mmoja.
Anasema kwa
mujibu wa Sheria za Uchaguzi 2015, mtu akihukumiwa kifungo chini ya
mwaka mmoja, hawezi kupoteza sifa za kuwa kiongozi wa wananchi, hivyo
ndiyo sababu Nkulu ameweza kupata udiwani licha ya kuhukumiwa kwenda
jela.
Akata rufaa na kuachiwa
Diwani
huyo wa Kata ya Lusaka, anayetajwa kuwa mwanasiasa mkongwe asiyekubali
kushindwa, aliachiwa huru Desemba 16, mwaka jana, siku 54 tangu
alipohukuma kifungo na kukaa gerezani.
Akiwakilishwa
na mwanasheria wa kujitegemea, Bartazari Chambi, Nkulu alikata rufaa
Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, ambako aliwasilisha hoja tatu za
kukata rufaa.
Hoja yake
ya kwanza ilikuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya Sumbawanga iliyomtia
hatiani haikuthibitisha pasipo kuacha shaka kwamba walipigana na
mwenzake hadharani, hoja ambayo Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga iliona
haina mashiko.
Hoja
nyingine ni kwamba mahakama ilikosea kumhukumu kifungo cha miezi sita
jela, ambacho kwa kosa la aina yake ni adhabu ya juu wakati yeye
alitenda kosa hilo kwa mara kwanza.
Hata
hivyo, kabla kukata rufaa, Mahakama Kuu iliitisha jalada la kesi hiyo
ili kujiridhisha iwapo mahakama ya chini yake ya Hakimu Mkazi ngazi ya
Wilaya ya Sumbawanga kama ilitenda haki katika kutoa hukumu hiyo.
Hoja
yake ya tatu alidai mahakama haikupa mbadala katika kutoa hukumu kwa
kosa la aina hiyo, sheria inaelekeza hukumu ya kulipa faini ya Sh 500 au
kifungo cha chini ya mwaka mmoja.
Hata
hivyo, katika shauri hilo ambalo upande wa Serikali iliwakilishwa na
Mwanasheria Njoloyota Mwashubila, mahakama ya juu iliona adhabu
aliyopewa mshtakiwa huyo ilikuwa kubwa kuliko kosa na kwa kuzingatia
kuwa hilo ni kosa la kwanza kwa mkosaji.
Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Kakusuro Sambo anaeleza
kwamba kwa kuzingatia mazingira ya kosa na tukio, mahakama imempunguzia
adhabu kutoka kifungo cha miezi sita jela hadi mwezi mmoja na siku 24,
adhabu ambayo ilikwisha Desemba 16 mwaka jana.
Kwa
mantiki hiyo sasa, Nkulu alikaa gerezani siku 54, badala ya miezi sita
kama ambavyo iliamriwa awali na baada ya kutoka gerezani, aliapishwa na
kuendelea na shughuli za kuwatumikia wananchi kwa nafasi yake ya
udiwani.
Ndugu, viongozi, wananchi wamzungumzia
Mtoto
wa kwanza wa Nkulu, Elizabeth Ameir Nkulu aliyezungumza kwa niaba ya
familia anasema hukumu kwa baba yao iliwaathiri kisaikolojia kwani
hawakutegemea kwamba ipo siku angeweza kufungwa jela.
“Mzee
alikuwa kiungo katika familia ilituumiza sana, sasa tuna amani na
furaha tele. Shukrani zetu ziende kwa wale wote waliofanikisha kwa namna
moja au nyingine mzee wetu kutoka gerezani,” anasema.
Mbunge
wa Jimbo la Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka anasema Nkulu
kuchaguliwa kuwa diwani akiwa gerezani ulikuwa mpango wa Mungu na
kielelezo kwamba haki ya mtu hainyang’anywi.
Mbunge
huyo anawataka wakazi wa kata hiyo kuweka itikadi za kisiasa kando na
kumuunga mkono Nkulu kwenye harakati zake za kuiletea maendeleo kata yao
ili iwe ya mfano wa kuigwa.
Naye
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Mkoa wa Rukwa, Aida Khenan anasema
kitendo cha wananchi kuchagua Nkulu akiwa gerezani inaonyesha namna
walivyo na imani naye, hivyo ni wajibu wake akiwa kiongozi wa wao
kuhakikisha anamaliza kero zao kwenye afya, maji na elimu.
Mkazi wa Kijiji cha Kizumbi, Kenta Said anasema alifanya uamuzi kumchagua diwani huyo kwa kuwa katika miaka ya nyuma aliweza kuwasaidia kutatua kero mbalimbali zinazowakabili aliposhika nafasi hiyo.
Anataja
matatizo yaliyowaandama ni pamoja na ukosefu wa maji, dawa kwenye
zahanati na vituo vya afya hivyo wamemchagua ili akashughulikie matatizo
hayo.
Mkazi wa Kata ya
Lusaka, Jephari Minazi anasema diwani Nkulu ni kielelezo cha
wapambanaji na wapenda maendeleo, wasiokubali kudhulumiwa haki zao akiwa
mstari mbele pia kudai haki za wanyonge ndiyo sababu wanachi walichagua
akiwa gerezani.
“Kumchagua
Nkulu tulikuwa sahihi kwani ndiye mtu anayeweza kutatua kero zetu
kwenye kata yetu ya Lusaka ambayo ina changamoto mbalimbali zikiwamo za
afya, elimu na maji,” anasema.
Nkulu alonga
Alipotakiwa
kueleza anavyojisikia baada ya kutoka gerezani akiwa diwani, Nkulu
anasema: “Najisikia mwenye furaha na amani moyoni baada ya kushinda
rufaa yangu, lakini kilichonifurahisha zaidi ni namna wananchi wa kata
yangu walivyokuwa na imani nami hata kujitokeza kwa wingi kupiga kura na
kunichagua wakati natumikia kifungo gerezani.”
Anaongeza
kwa kusema kuwa: “Wananchi wameonyesha upendo kwangu. Nina deni kubwa
kwao la kuhakikisha kata inapata maendeleo endelevu na ni wajibu wangu
kuhakikisha nalipa deni.”
Anasema kuchaguliwa kwake akiwa gerezani pia ni fundisho katika jamii kwamba haki itabaki kwa mwenye haki.
“Sijui
kama yupo diwani au kiongozi mwingine nchini aliyechaguliwa akiwa
gerezani kama ilivyokuwa kwa mimi; kama hayupo basi miye ni mfano wa
kuigwa na somo kwa watawala,” anasema Nkulu.
Hata
hivyo, Nkulu hakuwa tayari kuzungumzia maisha ya gerezani yalivyo huku
akisisitiza hawezi kukubali kuona mwananchi kwenye kata yake anafungwa
jela, bali atahakikisha anasimamia haki inatendeka kwa wananchi wake
wote.