Membe, Sitta, Wasira, basi tena kwa Magufuli *Wafungiwa vioo bungeni, wizarani *Wamo Mwandosya, Migiro, Mukangara, Sophia Simba aponea cheo chake UWT
Katika safu yake hiyo iliyokamilika mwishoni mwa wiki baada ya
kuwaapisha makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu Ikulu jijini Dar es
Salaam, Rais Magufuli aliendelea kutoa nafasi zaidi kwa sura mpya huku
akiachana na majina kadhaa maarufu ya watu waliowahi kuongoza wizara
katika serikali ya awamu ya nne ya Rais Kikwete, wakiwamo Bernard Membe
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Usbirikiano wa Kimataifa, Samuel
Sitta wa Wizara ya Uchukuzi, Stephen Wasira wa Kilimo, Chakula na
Ushirika na pia Prof. Mark Mwandosya. Baadhi ya vigogo hao wa serikali
iliyopita, akiwamo Sitta ambaye pia aliwania Uspika bila mafanikio,
wamekaririwa wakisema kuwa sasa wamestaafu rasmi siasa.
Membe, Sitta, Wasira na Dk. Asha-Rose Migiro aliyekuwa Waziri wa
Sheria na Mambo ya Katiba, ni miongoni mwa makada 38 wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) waliojitosa katika mchakato wa kuwania kuteuliwa kuwa
wagombea urais wa chama chao (CCM) ambao mwishowe Magufuli ndiye
aliyeibuka mshindi.